Latest Post
Showing posts with label historia. Show all posts
Showing posts with label historia. Show all posts
11:39
Mwisho ningependa kumwekea Waislam waliopata misukosuko wakati wa utawala wa Nyerere. Nafanya hivi kwa kuwa yeye anadai Waislam hawakutaabishwa na Waingereza. Ukweli ni kuwa Waingereza na Watanganyika waliendesha siasa za upole tofauti na Kenya. Matatizo kwa Waislam na Uislam yalikuja baada ya uhuru mwaka 1961. Hawa wafuatao ndiyo waliofungwa na Nyerere:Abdillah Schneider Plantan, Sheikh Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Shariff Hussein Badawiy, Shariff Mwinyibaba, Shariff Adnan, Bilali Rehani Waikela, Sheikh Jumanne Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh Hashim Haji Abdallah, Sheikh Nurdin Hussein, Salum Abdallah Popo (babu yake Mwandishi), Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al Amin Maftah, Rajab Kiguu cha Mbuzi, Ahmed Rashad Alina wengine wengi.
Juu ya hayo yote Tanzania ni nchi huru watu wana uhuru wa kumpachika yeyote wampendae jina wanaloona linamwenea ama liwe “Baba wa Taifa,” “Baba wa Kanisa” nk. Mtu huwezi kuwa na ugomvi na mambo kama haya. Leo kuna maprofesa wala hawajauona mlango wa darasa na maprofesa hawajaenda mahakamani kuweka p;ingamizi wala wenye shahada zao hawajaonesha kukereka. Ukipenda unaweza hatakuwa Field Marshal na hakuna atakaekuuliza wapi ulipigana vita na katika jeshi lipi. Halikadhalika mtu ana uhuru wa kuamini historia yoyote aitakayo. Anaweza kudai kuwa TANU ilianzishwa na Nyerere mwaka 1954 na akaja mwingine akasema hilo haliwezekani na kama kuna mzalendo anaeweza kujinasibu na kuanzishwa kwa TANU basi marehemu Abdulwahid Sykes anastahili zaidi kwani baba yake ndiye aliyeasisi African Association mwaka 1929 na kati ya 1930 hadi 1933 akajenga ofisi ya African Association New Street, nyumba ambayo TANU ilikuja kuzaliwa ndani yake mwaka 1954.
Uhuru wa Tanganyika Haukuletwa na Nyerere Peke Yake Mohamed Said
Written By mahamoud on Monday, 30 December 2013 | 11:39
Uhuru wa Tanganyika Haukuletwa na Nyerere Peke Yake
Mohamed Said
Kama kawaida ya makala za Mzee wangu Yusuf Halimoja huwa ni mchuzi wenye viungo vingi, hiliki, giligilani, abdalasini, binzari nyembamba na kadhalika. Mzee Halimoja kazungumza kuhusu historia ya TANU na nafasi ya Nyerere, kazungumza kuhusu Mihadhara ya “Uchochezi ya Waislam,” kazungumza kuhusu Elimu ya Waislam na Chuo Kikuu, kama ada yake hakuweza kuacha kuzungumza kuhusu Waarabu na Utumwa, nk. (Jamhuri 17 23, 2012) Insha Allah nitajitahidi kugusa kote. Pili ningependa kumfahamisha Mzee Halimoja kuwa hicho kichwa kilichopamba makala yangu aliyoijibu, “Halimoja ana Chuki na Waislam,” si kichwa nilichoandika mimi. Nadhani kichwa hiki ndicho kilichomfanya Mzee Halimoja aseme kuhusu “uchochezi” wangu. Sasa ikiwa mimi sikuweka kichwa hicho hapo awali ni wazi kuwa shutuma ya uchochezi itakuwa imeniepuka isipokuwa nitabakia na lile la kuwaenzi Waislam na mchango wao katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Hata hivyo hilo halinitoi katika kujibu baadhi ya shutuma kuhusu Waislam kuwa ni “wachokozi.”
Napenda kumfahamisha Mzee wangu Yusuf Halimoja kuwa kuwa katika maandiko yangu yote na katika mihadhara niliyopata kutoa ndani na nje ya nchi sijapata kusema kuwa Waislam walitoa mchango mkubwa kuliko mchango alitoa Nyerere katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Sijaona haja ya kupima nani kasaidia zaidi harakati za kudai uhuru labda kwa kuwa hata kama leo nitataka kufanya hivyo tatizo litakuwa ni vigezo gani nitumie ili kujua nani kamzidi nani. Hii bila shaka itakuwa kazi kubwa kwa kuwa walipogania uhuru wa Tanganyika walikuwa wengi. Kuna wale waliokuwa pale Makao Makuu ya TAA na kasha TANU pale New Street, Dar es Salaam na kuna wale waliokuwa majimboni. Jingine ni kuwa hadi TANU inaanzishwa TAA ilikuwa tayari ishakuwapo kwa miaka 21 na viongozi wakiingia na kutoka na kila mtu alikuwa na mchango wake. Mzee Halimoja akitaka kujua mchango wa viongozi hawa ambae yeye hawaoni kuwa ni wanasiasa na asome tahariri alizokuwa akiandika katika miaka ya 1930 ndani ya gazeti lake alilokuwa kilihariri yeye mwenyewe, “Kwetu.” Nakala za gazeti hili zinapatikana Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Fiah alikuwa mfuasi wa Marx na alijaribu kuhamasisha tabaka la wafanyakazi na wakulima kuwaunganisha dhidi ya ukoloni. Kuanzia mwaka wa 1950 kulikuwa na kamati ya ndani ya TAA iliyokuja kuasisi TANU. Pamoja na haya kuna viongozi wa Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika waliokujatoa uongozi katika TANU. Sasa vipi mtu atasema harakati kazianza Nyerere wakati haya yalipokuwa yakitendeka Nyerere hakuwapo? Kuna wazalendo kama Kleist Sykes, Ali Jumbe Kiro, Ali Mwinyi Tambwe, Salum Abdallah, Ibrahim Hamisi, Hassan Machakaomo Maalim Popo Saleh na wengine, hawa waliitumikia African Association, kasha TAA na baadae TANU. Wengi wao walishughulika sana katika miaka ya 1940 hadi kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili. Kuna watu kama Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz (wanakamati ya ndani ya TAA) waliokuja kupokea kijiti kutoka kwa wazee wao. Dossa alikuwa hapandi jukwaani lakini ndiyo ilikuwa “benki” ya TANU. Inasemekana hakuna wa kumfikia Dossa kwa fedha alizotoa katika kupigania uhuru. Ikutoshe tu kuwa gari la kwanza TANU kuwanalo kumsaidia Nyerere kwenda huku na kule alilitoa Dossa. Abdulwahid Sykes hakuwa anapanda jukwaani lakini na yeye alikuwa “sanduku la fedha” la TANU, halikadhalika mdogo wake Ally Sykes.
Kalamu ya Abdulwahid Sykes na mipango alokuwa akiipanga akishirikiana Mufti wa Tanganyika na Zanzibar Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu, Dk. Vedasto Kyaruzi, Stephen Mhando na wanakamati wa TAA Political Sub Committee ndiyo iliyosababisha uhuru upatikane mwaka 1961. Kamati hii iliundwa 1950 ndani ya TAA na wakati ule Nyerere hakuwapo. Vijana hawa walikungwa mkono na wazee waliounda Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa na Waislam watupu. Katika hawa wazee wapo waliokuwa wanapanda majukwaani na kusafiri na Nyerere vijijini kuitangaza TANU kama Sheikh Suleiman Takadir, Rajab Diwani na wengineo na walikuwapo wengine hawakuwa wapanda majukwaa lakini wakichangia juhudi zile kwa njia nyingine. Katika hawa mchango wa Mshume Kiyate ni wa kupigiwa mfano. Harakati za kudai uhuru hazikuanza na Nyerere mwaka 1954 vuguvugu lilianza toka miaka ya mwisho ya 1920 African Association ilipoasisiwa. Chama hiki kina historia yake na kina mashujaa wake waliofanya makubwa, katika wakati wao kama Kleist Sykes, Erika Fiah, Ali Juma Ponda, Hassan Tawafiq Suleiman, Edward Mwangosi na wengine wengi. Wazalendo hawa walikuwa na mchango wao wa kuwaamsha wananchi wajijue.
Naamini Mzee wangu Halimoja labda hakuwa anayajua haya kama Watanzania wengi walivyokuwa gizani katika historia hii ya kutukuka. Mzee Halimoja yeye anaamini hapakuwa na siasa katika TAA lakini Waingereza wakijua fika kuwa TAA ingawa haikuwa na katiba ya siasa lakini kilikuwa chama cha siasa kamili. Moja ya masikitiko yangu ni kuwa hadi leo watoto wa marehemu Abdulwahid Sykes hawajaamua kuzifungua na kuziweka wazi shajara zake alizokuwa akiziandika wakati kabla na baada ya kuunda TANU kwa hiyo mengi hayajulikani kama ambavyo tungelipendfa kufahamu. Ningependa kumwekea msomaji hapa machache kutoka nyaraka za Sykes:
"...it is reported that the Secretary of the Association, Abdul Wahid Sykes has
dispatched letters to all branches asking members for suggestions under
the following heads for a memorandum to be prepared for the Royal
Commission..."
“...Abdul Wahid Kleist Sykes, Secretary of the African Association who, as
reported in last month's summary (paragraph 20) was going on safari up
country, visited Mwanza, where he met Paul Bomani, President of the
Bukoba African Association, and accompanied him to Bukoba. Sykes then
visited Kampala alone.....on 8th March, a secret meeting was held, attended
by leading members of the Mwanza Branch...”
(Tanganyika Political Intelligence Summary March, 1952).
by leading members of the Mwanza Branch...”
(Tanganyika Political Intelligence Summary March, 1952).
Tukija katika TAA hasa kuanzia mwaka wa 1950 kuna wengi waliopambana na ukitaka kujua hali ya siasa ilivyokuwa wakati ule pitia nyaraka za marehemu Abdulwahid Sykes. Utakayosoma katika nyaraka hizi zitakudhihirishia bila hofu wala wasiwasi kuwa TAA kilikuwa chama cha siasa. Kutokana na nyaraka hizi mwandishi ameandika kitabu cha maisha ya Abdulwahid Sykes na ndani yake kawataja wale wote walioondolewa aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya katika historia ya kudai uhuru. Inawezekana watu kama Halimoja hawataki tu kusikia upande mwingine wa historia. Hili ni jambo la kusikitisha kwani kwa kuifunga akili yao kuhusu historia hii watapitwa na mengi. Halimoja anasema Nyerere ndiye aliyepeleka harakati vijijini. Halimoja anasema hivyo kwa kuwa labda kama ni mkweli kuna asiyoyajua kuhusu kuipeleka TANU kwa wananchi. Ushahidi wa kihistoria haukubaliani na msimamo wa Mzee Halimoja. Ningependa kumkumbusha Mzee Halimoja majina ya waasisi wa African Asociation kwa kuwa yeye kanasa na Cecil Motola peke yake mtu wa Masasi mwenzake. Kleist Sykes ndiye aliyeasisi Africa Association baada ya kuifanyia kazi fikra aliyopewa na Dr. Aggrey mwaka 1924. Kleist aliasisi African Association mwaka 1929 akiwa na rafiki zake wa karibu kama Mzee bin Sudi, ambaye wazazi wake walikuwa Wamanyema kutoka Belgian Congo, Ibrahim Hamis - Mnubi ambaye baba yake alitoka Daffur nchini Sudan, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima - Mzaramo, Suleiman Majisu, Raikes Kusi, Rawson Watts na Cecil Matola - Myao kutoka Masasi, Kleist akiwa katibu muasisi wa African Association.
Napenda tena kumjuvya Mzee Halimoja kuwa wanachama wa kwanza wa TANU walitoka Rufiji mwaka 1954 na aliyekwenda kuwatafuta wanachama hao ni Said Chamwenyewe baada ya kuagizwa na Abdulwahid Sykes ili TANU ipate tasjila kwa kuwa wakoloni walikataa kuisajili TANU ati chama hakina watu. Katika kipindi hicho majuma machache tu tangu TANU iasisiwe Zuberi Mtemvu akachukua kadi za TANU kutoka kwa Ally Sykes akifuatana na Nyerere wakenda Morogoro kukitangaza chama. Mwaka 1956 katika vijiji vya Dodoma TANU iliingizwa vijijini na Haruna Taratibu na Omar Suleiman. Mwaka huo huo katika vijiji vya Jimbo la Kusini, TANU iliingizwa vijijini na Salum Mpunga, Yusuf Chembera, Suleiman Masudi Mnonji, Shariffa bint Mzee, Said Alley Mwalimu, Mohamed Ali Abdallah na wanaharakati wengine. Huko Kilimanjaro TANU ilienezwa na akina Yusuf Olotu, Mama bint Maalim, Halima Selengia, Melkezedek Saimon, Gabrieli Malaika, Eikaeli Mbowe, Juma Ngoma na wengine wengi. Mifano naweza kuitoa mingi sana.
Halimoja anasema labda kwa kegemea historia ya Nyerere kama aijuavyo yeye kuwa tawi la Dar es Salaam la TANU ndilo lilikuwa dhaifu. Sijui anakusudia tawi lipi kwa kuwa matawi ya TANU Dar es Salaam yalikuwa lukuki na yote hayo yalikuwa na nguvu sana kuanzia Makao Makuu New Street hadi uje Tawi la Kisutu ambalo baadae lilikuja kuhamia Mtaa wa Mvita. Hili tawi la Mvita lilikuwa chini ya uongozi wa Mtoro Kibwana kama katibu na Sheikh Haidar Mwinyimvua kama Mwenyekiti na baadae uenyekiti ukashikwa na Yahya Saleh. Inasemekana tawi hili ndilo lililokuwa na nguvu kushinda matawi yote Tanganyika. Huu ndiyo ukweli na picha na nyaraka kuthibitisha haya yote zipo na mwandishi katika kutafiti historia ya uhuru wa Tanganyika kapata bahati ya kuzisoma nyaraka za wakati huo na kuzifanyia uchambuzi. Sasa kama Mzee Halimoja bado kaelemewa na ile propaganda kuwa TAA kilikuwa chama cha starehe hakuna wa kumzuia katika fikra zake hizo. Kwa mukhtasari hii ndiyo ilikuwa michango ya baadhi ya wazalendo ambao hadi leo taifa limewasahau. Katika hali kama hii vipi Mzee Halimoja atadai kuwa Nyerere alikuwa na mchango wa pekee? Hiyo pekee kama ipo na ataufahamishe tupo tayari kumwazima masikio yetu.
Nampa chamgamoto Mzee Halimoja aeleze ni akina nani waliingiza TANU Peramiho na Masasi. Mtu mmoja asingeweza kupigana vita ile peke yake. Nyerere hakuwa peke yake si Dar es Salaam wala huko vijijini alikosema Mzee Halimoja. Tabu ya wanaotaka kumtukuza Nyerere peke yake kama Mzee Halimoja iko hapa. Wao hawawataki kabisa kusikia historia ya waliomtangulia Nyerere katika siasa au aliokuwanao pamoja bega kwa bega. Hamu yao kubwa ni kuwa historia ya uhuru wa Tanganyika ianze na kumalizikia kwa Nyerere. Iwe itakavyokuwa mimi sina ugomvi na wao kila mtu ana uhuru wa mawazo yake hatulazimishani katika hilo. Jambo la kushangaza ni kuwa anapokuja mtu na maelezo mengine ya historia ya kudai uhuru hawa wenzetu wanaumwa sana. Ninachosema siku zote ni kuwa uhuru wa Tanganyika umepiganiwa kwa kiasi kikubwa sana na Waislam na jambo la kusikitisha hao walioupigania uhuru huo bega kwa bega na Nyerere hawatambuliwi na hawajapewa heshima na hadhi wanayostahili. Haya ndiyo mambo mawili ambayo nimekuwa nikikisisitiza siku zote.
Sasa tuje suala la mihadhara. Historia ya mihadhara ni ndefu na inahitaji makala maalum ili kuitendea haki. Wachungaji walikuwa wakipita katika nyumba za Waislam kuwahubiria wakumkubali Yesu ili waokoke. Hili limekuwa likifanyika kwa zaidi ya miaka mia sasa. Kuna kisa maarufu cha Sheikh Idrissa bin Saad na padre kutoka kanisa la Misheni Kota aliyekuwa akija nyumbani kwa Sheikh Idrissa kumuhubiria “Neno la Bwana.” Inasemekana Sheikh Idrissa alikuwa akimkaribisha huyu mchungaji na akiagiza chai iletwe kwa jili ya mgeni wake na sheikh akikaa kimya kumsikiliza hadi amalize mahubiri yake kisha wanaagana. Wanafunzi wa sheikh walikuwa wakikereka sana na hali ile lakini Sheikh Idrissa alikuwa akiwaeleza kuwa dini inahitaji ustahamilivu. Kwa muda mrefu sana mahubiri ya dini yalikuwa yakifanywa na Wakristo peke yao na kwa kweli mihadhara hiyo haikuwa na athari yoyote kwenye Uislam. Matatizo yalianza pale Waislam kuanzia miaka ya mwanzo 1990 nao walipoanza kutoka misikitini na kuutangaza Uislam hadharani wakitumia Biblia. Baada ya mihadhara hii huko Sumbawanga Wakristo 2000 kutoka Kanisa Katoliki walisilimishwa na Kagera Padri Yusufu Makaka wa Kanisa la Kilutheri Kagera yeye na wafuasi wake 3000 walisilimu na kuingia Uislam. Hofu kuu iliingia katika kanisa na hawakuwa na pa kwenda isipokuwa kuomba msaada wa seriakali ilihami kanisa lisije likasambaratika. Kadinali Otunga wa Kanisa Katoliki Kenya yeye alitoa ilani kwa kusema kuwa kanisa lipo katika hali ya kusambaratishwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kulihami dhidi ya wahubiri wa Kiislam. Kufuatia matokeo haya mwaka 1989 Christian Council of Tanzania (CCT) iliionya serikali kuhusu wahubiri wa Kiislam. Mwaka 1993 Tanzania Episcopal Conference (TEC) ikatoa taarifa yenye vitisho kuwa endapo Waislam hawataacha mahubiri yao damu itamwagika. Mapdri walijaribu kupambana na wahubiri wa Kiislam juu ya ulingo lakini walikuwa wanashindwa vibaya sana. Hilo ndilo lilowafanya wakimbilie kutoa vitisho na kutaka msaada wa serikali kuwadhibiti Waislam. Mtokeo ya juhudi hizi za kanisa ni mauaji ya Mwembechai mwaka 1998. Hii ndiyo hali ya mambo kwa mukhtasari.
Mzee Halimoja kaeleza habari ya Waarabu na utumwa. Hakuna wa kupinga hilo kuwa Waarabu walishiriki katika biashara ya utumwa kama vile walivyoshiriki Wazungu na Waafrika. Hata hivyo ningependa kumzindua kuwa mbona kawataja Waarabu peke yao katika biashara hii? Kwani yeye hajui kuwa kulikuwa na biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlantic na meli moja ya kubeba watumwa ilikuwa ikiitwa “Jesus?” Mzee Halimoja kaeleza Waislam kukosa chuo kikuu hadi walipopewa na Benjamin Mkapa. Kisa cha East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kupigwa kwake marufuku na Nyerere ni katika mambo maarufu kwa Waislam. Mzee Halimoja anatonesha kidonda. Nyerere aliihujumu jumuia hiyo ya Waislam kwa kuwa ilikuwa ikijenga Chuo Kikuu. Mkapa akitumia gazeti la Nationalist, Martin Kiama akitumia Radio Tanzania, Geofrey Sawaya wa Jeshi la Polisi walikuwa washiriki wakuu wa katika kampeni ile dhidi ya EAMWS mwaka 1968 kama lilivyokuwa Kanisa Katoliki wakimtumia Nyerere. Hii ni mada ya kujitegemea Insha Allah itakapopatikana nafasi tutazungumza kwa marefu na mapana yake.
Juu ya hayo yote Tanzania ni nchi huru watu wana uhuru wa kumpachika yeyote wampendae jina wanaloona linamwenea ama liwe “Baba wa Taifa,” “Baba wa Kanisa” nk. Mtu huwezi kuwa na ugomvi na mambo kama haya. Leo kuna maprofesa wala hawajauona mlango wa darasa na maprofesa hawajaenda mahakamani kuweka p;ingamizi wala wenye shahada zao hawajaonesha kukereka. Ukipenda unaweza hatakuwa Field Marshal na hakuna atakaekuuliza wapi ulipigana vita na katika jeshi lipi. Halikadhalika mtu ana uhuru wa kuamini historia yoyote aitakayo. Anaweza kudai kuwa TANU ilianzishwa na Nyerere mwaka 1954 na akaja mwingine akasema hilo haliwezekani na kama kuna mzalendo anaeweza kujinasibu na kuanzishwa kwa TANU basi marehemu Abdulwahid Sykes anastahili zaidi kwani baba yake ndiye aliyeasisi African Association mwaka 1929 na kati ya 1930 hadi 1933 akajenga ofisi ya African Association New Street, nyumba ambayo TANU ilikuja kuzaliwa ndani yake mwaka 1954.
Siwezi kumjibu Mzee Halimoja kila alosema hapa tulipofika panatosha.
19 Januari, 2012
19 Januari, 2012
| Sheikh Nurdin Hussein Khallifa wa Tariqa Shadhliy |
![]() |
| Ali Juma Ponda |
| Erika Fiah |
Labels:
historia,
investigative
10:26
Naweka hapa chini yale ambayo niliandika katika kitabu changu, ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...'' kuhusu Mzee Bilal Rehani Waikela:

Uongozi wa East African Muslim Welfare Society katika ni Solomon Eliufoo (Waziri wa Elimu) na Tewa Said Tewa (Territorial President EAMWS) kulia kabisa aliyevaa kanzu na kilemba ni Mufti Sheikh Hassan bin Amir.
BILALI REHANI WAIKELA...
Written By mahamoud on Friday, 27 December 2013 | 10:26
![]() |
| Bilali Rehani Waikela akitoka Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam alipokuja kutoa ushahidi kesi ya Sheikh Ponda |
Naweka hapa chini yale ambayo niliandika katika kitabu changu, ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...'' kuhusu Mzee Bilal Rehani Waikela:
''Napenda kutoa shukrani maalum kwa Bilal Rehani Waikela, muungwana wa Kimanyema na Muislamu wa kweli. Waikela akiwa na umri wa miaka ishirini na tano mwaka 1955, alikuwa mmoja wa waasisi wa TANU mjini Tabora. Waikela alinieleza jinsi Waislam kwa umoja wao walivyomuunga mkono Julius Nyerere na harakati za uhuru. Vilevile vilevile alinieleza kwa muhtasari siku zake kizuizini pamoja na babu yangu katika gereza la Uyui, Tabora kwa kile kilichoitwa kosa la ëkuchanganya dini na siasa.í Nina deni kubwa kwake kwa kunipa picha za wakati ule na nyaraka zake binafsi juu ya ëmgogoroí wa EAMWS uliozushwa mara baada ya uhuru. Natoa shukrani kwa Waikela kwa kunitia hima na kunipa moyo kuandika kitabu hiki ili nieleze kuhusu dhulma waliofanyiwa Waislam na utawala wa Nyerere. Waikela tofauti na watu wengine waliozungumza na mimi aliniruhusu pia kumnukuu kwa jina bila ya woga wowote. Alifurahi kuona kwamba historia ya kweli ilikuwa inaandikwa na habari alizonieleza zitakuja kutumika katika kuhifadhi historia ya nchi yetu kwa faida ya vizazi vijavyo. Vilevilevilevile Waikela alinikutanisha na wazalendo wengine kama Mohamed Mangiringi, marehemu Ramadhani Singo na wengineo ambao nilizungumzanao kwa kirefu.
Mwaka 1955 Bibi Titi Mohamed na Julius Nyerere waliitika mwaliko na kuja Tabora. Mkutano ulifanyika katika ile kilabu ya kandanda. Waliohudhuria mkutano ule walikuwa Germano Pacha, Juma Mrisho, Shaaban Mohamed Silabu, Bilali Rehani Waikela, Mohamed Mataka wakati ule akiwa muadhin wa Masjid Nur - msikiti wa Wamanyema pale Tabora, Hassan Mohamed Ikunji, Ramadhani Mussa Wajaku, Swedi Mambosasa, Said Ali Kiruwi na Hamis Khalfan. Uongozi wa kilabu ulimwambia Nyerere na Bibi Titi kuwa kilabu hiyo ya kandanda ilikuwa ikitaka udugu na TANU ili ifanye kampeni ya kuipatia TANU wanachama wengi. Uongozi huo wa TANU kutoka makao makuu Dar es Salaam uliambiwa kuwa maadam kilabu hiyo ilikuwa ikipendwa na kuungwa mkono na watu wa Tabora na ilikuwa maarufu sana, sifa hizo zingeweza kutumiwa kwa manufaa ya TANU. Vilevile Nyerere alifahamishwa kuwa kilabu hiyo ingependa kuvijumuisha vyama vitatu vya lelemama na vikundi vya taarabu, Nujum ul Azhar, Waridatil Hubb na Egyptian Club. Nyerere na Titi waliyakubali mapendekezo haya na usiku ule akifuatana na uongozi wa kilabu Nyerere alizungumza na kikundi cha watu waliyokusanyika nje ya nyumba ya kilabu juu ya hali ya Tanganyika katika siku zijazo. Nyerere alikuwa amerudi Tabora ambapo alianza siasa kiasi cha miaka minane nyuma. Jambo muhimu katika kipindi hiki pale Tabora ni kuwa wasomi wa Makerere waliokuwa St. Maryís School hawakuwapo katika harakati hizi na katika mikakati iliyokuwa ikipangwa.
Bibi mmoja wa Kiganda, Nyange bint Chande, mwanachama wa moja ya vikundi vya lelemama mjini Tabora alijitolea nyumba yake kama ofisi ya kwanza ya TANU katika Jimbo la Magharibi. Uchaguzi ulifanyika na Shaabani Marijani alichaguliwa Mwenyekiti wa Wilaya na Idd Said Ludete Katibu wa TANU. Bilali Waikela akawa mjumbe wa kamati. Kadi za kwanza za uanachama wa TANU ziliuzwa ndani ya soko la Tabora na Amani Idd na Pacha, Katibu wa Jimbo wa TANU. Pacha alikuwa na lingo la kuni pale sokoni kama biashara yake. Baadae Amani Idd alisaidiwa kazi hiyo ya kuuza kadi za TANU na Dharura bint Abdulrahman.
Makao makuu ya TANU yaliamua kumtuma Peter Mhando, (mdogo wake Stephen Mhando) kwenda Tabora kufanya uchunguzi na kuandika taarifa ambayo ingetoa msingi wa ufumbuzi wa kudumu kuhusu matatizo yanayoisibu TANU pale Tabora. Wakati ule Peter Mhando alikuwa kijana wa kiasi cha miaka ishirini hivi aliifanya kazi ile na vijana wengine kama Bilal Waikela, Ramadhani Abdallah Singo, Abdallah Saidi Kassongo na vijana wengineo. Vijana hawa walikamilisha taarifa na kuituma makao makuu. Hii ilikuwa ndiyo kazi ya mwisho ya Mhando kuifanyia TANU kwani alifariki kwa ugonjwa wa kisukari mara tu baada ya kutayarisha na kutuma taarifa yake makao makuu ya TANU.
Jaribio la mwanzo la Nyerere kutaka kuivunja EAMWS lilikuwa mwaka 1963. Lakini jaribio hilo halikufanikiwa kwa sababu ya mpango uliopangwa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir na kutekelezwa na Bilali Rehani Waikela, katibu wa EAMWS Tabora. Mwaka huu wa 1963 EAMWS ilifanya mkutano wake katika ukumbi wa Shule ya wasichana ya Aga Khan. Wajumbe wa mkutano huo walipowasili mjini Dar es Salaam walikuta uvumi kuwa wajumbe wa mkutano wa EAMWS watakamatwa na kuwekwa kizuizini. Chanzo cha uvumi huu hakikufahamika lakini haikuwa vigumu kuhisi. Baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka ule ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa amewatupa mkono washirika wake wa zamani na sasa alikuwa akitafuta wapya ili kujenga upya msingi wake wa siasa. Kutokana na mambo yalivyokuwa yakienda ilikuwa ni dhahiri washirika wake wapya hawatakuwa Waislam.
Katibu wa EAMWS Tabora, Waikela alipowasili Dar es Salaam kuhudhuria mkutano aliitwa na Sheikh Hassan bin Amir. Mufti Sheikh Hassan bin Amir mbele ya Mzee Ali Comorian, alimfahamisha Waikela kuwa kulikuwa na njama zilizokuwa zikipikwa na Nyerere kumuungamiza yeye na Tewa Said Tewa ili kuvunja EAMWS ipatikane nafasi ya kuanzishwa jumuiya ya Kiislam ya Watanganyika itakayokuwa chini ya wanafiki. Sheikh Hassan bin Amir alimwambia Waikela kuwa harakati za uhuru zilikuwa zinatekwa nyara na Wakristo kwa manufaa ya makanisa yao. Sheikh Hassan alimfahamisha Waikela kuwa ni lazima yeye afanye kila linalowezekana ili njama za Nyerere zishindwe. Waikela alimuuliza Sheikh Hassan bin Amir kwa nini amechaguliwa yeye kufanya kazi ile. Sheikh Hassan bin Amir alimuambia kuwa yeye ana imani na uwezo wake. Baada ya maneno hayo Sheikh Hassan bin Amir alinyanyua mikono yake juu na kumuombea dua Waikela. Nyerere alikuwa anamfahamu Waikela kwa kuwa alikuwa muasisi wa TANU na alikuwa ametoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru.
Nchi nzima hasa sehemu za Waislam kulikuwa mpango wa serikali wa kuwavunja Waislam nguvu na kuwakatisha tamaa. Waikela, kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wa EAMWS alikuwa anasuguana na Mkuu wa Mkoa wa Jimbo la Magharibi, Richard Wambura. Kulikuwa na ujeuri kwa upande wa serikali walipokuwa wanashugulikia matatizo ya Waislam, mbali na mategemeo ya Waislam waliyokuwanayo kabla ya uhuru. Subira ya Waikela ilifikia kikomo pale Wambura alipowatukana Waislam katika mkutano wa hadhara. Baada ya kuhutubia Wambura, Waikela alipanda jukwaani na akaikumbusha serikali isiwe mwizi wa fadhila kwa kusahau jinsi Waislam walivyojitolea muhanga katika kudai uhuru. Serikali ikachukulia hotuba ya Waikela kama usaliti na yenye kuwashawishi Waislam wasiitii serikali. Ilikuwa katika hali hii Waikela mwanachama shupavu wa TANU alijitoa kwenye chama na akaamua kutumia nguvu zake kuwatumikia Waislam kupitia EAMWS. Ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa na habari za msuguano kati ya serikali na Waislam kule Tabora na mtu ambae alikuwa akihusika na msuguano huo.
Siku kabla ya mkutano wa EAMWS, Nyerere aliwaalika wajumbe wa mkutano Government House kwa chakula cha usiku. Hao waalikwa walikuwa wajumbe waliochaguliwa mahsusi. Waikela hakuwa mmoja wa hao waalikwa. Nyerere alichukua nafasi ile kuwashauri wajumbe wale waanzishe jumuiya ya Waislam wa Tanganyika ichukue nafasi ya EAMWS. Wajumbe hawa walipoleta katika mkutano hoja ya kuanzisha jumuiya ya Waislam wa Tanganyika, Waikela alisimama na kuipinga hoja ile. Alizungumza vilevile kuhusu uadui wa serikali kwa Waislam na Uislam. Waikelaalimaliza hotuba yake kwa kutoa changamoto kwa wajumbe wamuite Nyerere kwenye ufunguzi wa mkutano ili aje awaeleze wajumbe msimamo wake kuhusu kadhia hii ya chinichini baina ya serikali na Waislam.
Baada ya kushindwa kwa hoja ya kuivunja EAMWS wajumbe wa mkutano ikaonekana kuwa ingekuwa vyema Nyerere aitwe kufunga mkutano ule na asomewe makubaliano yaliyofikiwa. Nyerere alifika kufunga ule mkutano na akakutana uso kwa uso na Waikela, ambae alimsomea maazimio ya mkutano. Waikela alimfahamisha Nyerere kuwa umoja kwa Waislam ni fardh ñ wajibu wa lazima. Ni kwenda kinyume na maamrisho ya Allah kuwagawa watu. Baada ya utangulizi huu Waikela huku akimnyooshea Nyerere kidole alieleza uadui unaoonyeshwa na serikali dhidi ya Waislam. Waikela alimaliza hotuba yake kwa kitisho. Alimwambia Nyerere ikiwa Waislam watamgeuka kupambana na yeye hatakuwa na uwezo wa kuwashinda. Nyerere alitulia tuli pembeni mwa Rais wa Baraza la Tanganyika la EAMWS Tewa Said Tewa akimsikiliza Waikela. Aliposimama kujibu hotuba ya Waikela Nyerere kwa upole alisisitiza msimamo wa serikali wa kutoa haki na usawa kwa raia wake wote.
Kwa kiasi fulani Nyerere alikuwa amefanikiwa kupunguza joto kati ya Waislam na serikali. Hotuba ya Waikela na ya Nyerere zikapewa umuhimu mkubwa katika radio. Waislam wengi wakajitokeza stesheni ya gari moshi Tabora kuja kumpokea shujaa Waikela. Alipewa heshima ile kwa kuwa na ujasiri wa kuweza kusimama kidete dhidi ya wale waliodhani kuwa wanaweza kuwakalia Waislam vichwani. Nyerere alihisi ameumbuka na hili lilimchoma moyo sana. Kuanzia hapa Nyerere hakumtazama Sheikh Hassan bin Amir kwa jicho jema. Alingoja nafasi yake ili alipize kisasi. Mwaka uliofuata, tarehe 20 Januari, 1964 jeshi liliasi. Nyerere alichukua fursa ile kuwatia kizuizini masheikh walioonekana wanapinga serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi. Waikela alikuwa mmoja wa wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. [1]Nyerere kwa wakati ule hakuwa na nguvu ya kumgusa Mufti Sheikh Hassan bin Amir...''
In Sha Allah Itaendelea...
Uongozi wa East African Muslim Welfare Society katika ni Solomon Eliufoo (Waziri wa Elimu) na Tewa Said Tewa (Territorial President EAMWS) kulia kabisa aliyevaa kanzu na kilemba ni Mufti Sheikh Hassan bin Amir.
11:13
MAPITIO YA KITABU SIMBA WA VITA KATIKA HISTORIA YA TANZANIA RASHIDI MFAUME KAWAWA
Written By mahamoud on Thursday, 26 December 2013 | 11:13
MAPITIO YA KITABU SIMBA WA VITA KATIKA HISTORIA YA TANZANIA RASHIDI MFAUME KAWAWA
Na Mohamed Said
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilishuhudia kuandikwa kwa historia ya mmoja wa viongozi wakuu wake kupitia kitabu “Simba wa Vita Katika Historia ya Tanzania Rashidi Mfaume Kawawa” kilichoandikwa na Dk. John M. J. Magotti. Sidhani kama katika historia ya Tanzania kuna kumbukumbu ya kuandikwa kwa kitabu kinachohusu maisha ya kingozi yoyote achilia mbali kufanyika kwa sherehe ya kukizindua kitabu hicho Ikulu ikiongozwa na rais mwenyewe. Kwa hakika sherehe ilifana sana na tukakisubiri kwa hamu kitabu madukani ili tupate kunufaika na kumbukumbu za Mzee Kawawa.
Msomaji anaweza kukisoma kitabu chote chenye kurasa 127 kwa muda wa saa moja akawa kakimaliza chote na atakapokiweka chini akawa hakubakia na chochote cha maana katika fikra yake. Kwa nini iwe msomaji asibaki na kumbukumbu yoyote ya kiongozi mkubwa kama Mzee Kawawa mtu aliyeshuhudia kwa macho yake mwenyewe harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika na si hivyo tu yeye mwenyewe ni mmoja wa wale waliopigania uhuru wa Tanganyika na kushika nyadhifa kubwa za uongozi chini ya Mwalimu Julius Nyerere. Kwa kawaida vitabu vya maisha ya viongozi hasa wapigania uhuru huwa vina mambo mengi sana ambayo kwa muda mrefu huwa siri, hayafahamiki hadi hapo kitabu kitakapoandikwa ama kwa mkono wake kiongozi mwenyewe au kuandikwa na muandishi. Mifano ipo mingi. Kitabu kama “Mahatma Gandhi” klichoandikwa na Robert Payne au “Long Walk to Freedom” alichoandika Nelson Mandela mwenyewe au “Seeds of Freedom” alichoandika Bildad Kaggia hakika unapomaliza kusoma vitabu hivi lazima urudi nyuma kufungua kurasa hapa na pale kuzisoma upya zile sehemu zinasosisimua.
Huwezi kupata haya katika kitabu cha Mzee Kawawa. Huwezi kuyapata haya kwa kuwa mwandishi hakuandika kitu. Hakuandika kitu si kama Mzee Kawawa hana historia ya kusisimua na kuwa hana mengi ambayo wengi hawayajui katika maisha yake, nadhani mwandishi hakuwezakuja na jipya labda kwa sababu hakufanya utafiti wa kutosha kuweza kuandika kitabu kinachomuhusu simba wa vita aneunguruma. Kuna msemo wa Kiswahili usemao “Aungurumapo simba mcheza ni nani?” Kwa hakika simba wa vita hakuunguruma kabisa katika kitabu hiki. Sijui lawama zielekezwe wapi.
Mimi simjui Mzee Rashidi Kawawa kwa kiwango cha kusema naweza kunyanyua kalamu na kufanya pitio la kitabu kilichoandikwa kuhusu yeye. Nathubutu kuandika kuhusu kitabu chake kutokana na kumjua kwangu mimi nikiwa kama mwandishi na mtafiti ambae katika kutafiti kwangu nimekutana na jina la Mzee Kawawa hapa na pale katika nyaraka zilizo katika hifadhi ya ukoo wa akina Sykes. Nitatumia uzoefu wangu huu kueleza yale niliyoyaona katika nyaraka hizi na ninayojua kuhusu Mzee Kawawa na kufanya tathmini kwa yale niliyoyasoma katika kitabu cha Magotti.
Miaka kama ishirini iliyopita nikiwa kijana mdogo nilipata hamu ya kuandika historia ya kudai uhuru wa Tanganyika . Sikuona mtu wa kumuendea isipokuwa Ally Sykes. Nilipomueleza kuwa nia yangu ni kuandika kitabu kuhusu marehemu kaka yake Abdulwahid Sykes (1924- 1968) Ally Sykes alinambia kuwa atanipa nyaraka zake zote nizipitie kisha ndiyo nakaenae chini kwa mahojiano ya ana kwa ana. Katika nyaraka alizonikabidhi ndani yake nilikuta barua ya mkono aliyoandika Rashid Kawawa mwaka 1952 kutoka Bukoba akimletea Ally Sykes aliekuwa Dar es Salaam. Barua hii ya Mzee Kawawa kwa Ally Sykes ilikuwa ikimfahamisha Ally Sykes hali ya siasa Kanda ya Ziwa. Hii barua hadi leo ipo katika nyaraka za akina Sykes. Nilipokaa na Ally Sykes kutaka maelezo ya barua ile aliyoandikiwa na Kawawa, Ally Sykes alinipa kisa hiki:
Mwaka 1951 nilichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA). Chama hiki kiliundwa mwaka wa 1927 kwa lengo la kuendeleza maelewano mazuri baina ya serikali ya Malkia na sisi watumishi Waafrika. Rashid Kawawa alikuwa mwana kamati. Mimi nilichaguliwa pamoja na Thomas Marealle kama rais wa TAGSA. Katiba ya TAGSA iliamuru uchaguzi wa kila mwaka, na mimin nilirudishwa madarakani kama katibu mara nne hadi Oktoba, 1954 nilipojiuzulu baada ya kuhamishwa kwenda Korogwe kama adhabu kwa kuwa miongoni mwa wale wanachama 17 waliounda TANU. Watu kadhaa walishika urais. Stephen Mhando na Dr Wilbard Mwanjisi wote hao waliwahi kuchaguliwa kuwa marais wa TAGSA. Miongoni mwa wanachama watendaji wa TAGSA walikuwa Dr Michael Lugazia na Rashid Kawawa ambao alichaguliwa kuwa katibu baada ya mimi kujiuzulu. Kupitia TAGSA, Kawawa alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Tanganyika Federation of Labour (TFL).
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulipokuja kuzuru Tanganyika Agosti, 1951 kwa mara ya tatu, vyama vyote viwili, TAA na TAGSA, viliwakilisha malalamiko kwa ujumbe huo. TAGSA iliwakilisha malalamiko yake kuhusu ubaguzi katika utumishi serikalini kwa mujibu wa kupanga mishahara kufuatana na rangi ya ngozi. Mshahara wa Mwafrika ulikuwa wa chini zaidi kuliko ule aliokuwa akipokea Mzungu au Muasia kwa kazi hiyo hiyo. Kwa mfano Mwandishi wa hati mkato Mzungu alikuwa akipata mshahara mkubwa kuliko Mwafrika aliyekuwa na shahada au digrii kutoka chuo Kikuu cha Makerere. TAGSA vilevile tulilalamika kuhusu kuajiri makarani wa kutoka India na hali walikuwepo Waafrika kutoka Afrika ya Mashariki na Nyasaland ambao wangeweza kujaza nafasi hizo kwa urahisi.
Vyama vyetu hivi viwili TAA na TAGSA viliwakilisha malalamiko haya tukifahamu fika kwamba Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya vifungu nambari 76 na 77 vya Umoja wa Mataifa ambavyo viliwekwa ili kuendeleza maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya nchi zilizokuwa chini ya udhamini. Kama mdhamini Uingereza ilitakiwa kuhimiza na kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa kwa wote bila kubagua kwa misingi yajinsia, lugha au dini. Lakini Uingereza ilikuwa ikipuuza vifungu hivi bila aibu. TAGSA tuliwakilisha malalamiko haya ili Umoja wa Mataifa ujue matatizo halisi ya ukoloni nchini Tanganyika .
Mimi nikiwa katibu wa TAGSA nilifuatilia serikalini masuala yaliyoainishwa ndani ya malalamiko yetu. Suala lililokuwa likituhangaisha sana wakati ule ilikuwa uajiri wa Wahindi kutoka India , jambo ambalo niliieleza serikali halikuwa na faida, maadam kulikuwako na Waafrika ndani ya nchi ambao wangeweza kujaza nafasi zile. Jambo hili lilikuwa likisababisha manugíuniko makubwa miongoni mwa Waafrika. Hakuna majibu maridhawa yaliyopatikana kutoka kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa. Barua tulizoandika serikalini juu ya masuala hayo zilipuzwa na Chief Secretary, Bruce Hutt. Katika kufuatilia malalamiko haya, Niliandika barua moja kali sana na kwa mara ya kwanza bila kutafuna maneno niliuliza uhalali wa Waingereza kututawala Waafrika wa Tanganyika . Nillimwambia Katibu Mkuu kuwa kwa kuwa serikali imeshindwa kupata ufumbuzi kwa matatizo ya Waafrika, Uingereza lazima ijitoe Tanganyika na Umoja wa Mataifa utawale Tanganyika . Barua hiyo ilimkasirisha Katibu Mkuu na siku chache baadaye nilipokea barua kutoka serikalini iliyokuwa imejaa vitisho, dharau, stihizai na makemeo. Nikajibiwa kuwa hakuwa na suala la Umoja wa Mataifa kutekeleza utawala wa moja kwa moja Tanganyika .
Dkt Mwanjisi alikuwa amegusa suala nyeti sana kwa kuzungumzia matatizo ya ubaguzi wa rangi uliokuwa ukitukabili Waafrika wa . Kawawa, kama mjumbe wa kamati, akaniandikia barua akanitahadharisha nisichapishe ile hotuba ya Dkt Mwanjisi katika jarida la TAGSA bila idhini ya kamati ya utendaji. Kufuatia majibishano haya kati ya TAGSA na serikali, Dkt Mwanjisi kama alivyofanyiwa Dk Kyaruzi kabla yake, akahamishwa kutoka hospitali ya Sewa Haji mjini Dar es Salaam hadi Kingolwira Prison Hospital karibu na Morogoro. Kawawa na yeye akapewa uhamisho kwenda Bukoba na mimi nikapewa uhamisho kwenda Mtwara. Dk Mwanjisi na Kawawa walikubali uhamisho wao na wakaondoka Dar es Salaam . Mimi nilikataa uhamisho na nikabakia Dar es Salaam kupinga uhamisho wangu.
Alipokuwa Bukoba ndipo Kawawa akamwandikia Ally Sykes barua ile ya mwaka 1952 akimweleza hali ya siasa kama alivyoikuta Kanda ya Ziwa. Huyu ndiye Kawawa niliyemjua mimi kupitia nyaraka na mahojiano na Ally Sykes. Kwa kweli inasikitisha kuwa Dk Magotti hakupata fursa ya kuziangalia nyaraka hizi muhimu sana katika siyo historia ya Kawawa bali katika historia ya kuundwa kwa TANU na kudai uhuru wa Tanganyika . Endapo angepata nafasi ya kuziona hizi nyaraka zingempelekea katika kuwajua wazalendo wengine waliotajwa mle ndani kama Dk. Kyaruzi, Dk. Wilbard Mwanjisi ambao Kawawa alikuwanao katika harakati za TAGSA. Katika majina hayo angeweza kudodosa mengi kutoka kwa Mzee Kawawa na hivyo kuandika yale ambayo hayafahamiki kwa wengi. Hii imgekifanya kitabu kiwe cha maana.
Mathalan Kawawa angeeleza mtafaruku kati ya Mwalimu Nyerere na Dk. Mwanjisi nini chanzo chake na nini ikajakuwa matokeo yake. Halikadhalika angempa fursa Mzee Kawawa kumuhadithia mchango wa Dk. Michael Lugazia katika kuasisi kwa TANU hasa kipindi kile cha 1953 wakati TAA ilipokuwa inatayarisha rasimu ya katiba ya TANU. Kwa ufupi ni kuwa Dk Lugazi alikuwa akijaribu kuamsha ari ya TAA Bukoba ari iliyokufa kutokana na kufungwa kwa kiongozi wa TAA Bukoba Ali Migeyo. Kisa cha Ali Migeyo ni moja ya visa vinavyosikitisha sana katika historia ya Tanganyika kwani aliwekwa kizuizini na Mwalimu Nyerere kama alivyofungwa na Waingereza. Haiwezekani kuwa Kawawa asiwe na habari na kile kilichopelekea mpigania uhuru hodari kama Ali Migeyo aishie jela tena wakati nchi ikiwa huru. Migeyo alifungwa na wakoloni kwa kuwahamasisha Watanganyika kudai uhuru labda Mzee Kawawa angeulizwa angeeleza ni nini kilitokea wakaamua kumfunga Migeyo kama walivyomfunga Waingereza.
Kitabu kimegusia kazi alofanya Kawawa kama mtumishi wa serikali ya kikoloni katika kambi za raia wa Kenya walioshukukiwa kuwa ni Mau Mau. Katika hawa wafungwa walikuwawepo wananchama wa TANU ingawa hawa walikuwa Wakenya. Maarufu katika hawa alikuwa Dome Okochi Budohi (ambae kadi yake ya TANU ilikuwa na 6) na Patrick Aoko. Budohi alicheza senema pamoja na Kawawa iliyoitwa “Wageni Wema.” Kawawa na Budohi walikuwa wakifahamiana vizuri sana kwa sababu wote walikuwa wasanii. Budohi alikuwa mmojawapo katika bendi ya vijana wa mjini iliyojulikana kama Skylarks. Bendi hii baadaye ilibadilisha jina na kuitwa Blackbirds. Matangazo ya radio yalipoanza Tanganyika, Blackbirds midundo ya Blackbirds ilikuwa haikosekani kusikika radioni katika Sauti ya Dar es Salaam. Kawawa kama walivyo vijama wote wa Dar es Salaam wa wakati ule alikuwa mmmoja wa wapenzi wa bendi hii na alikuwa hakosekani Ukumbi wa Arnatouglo bendi hii ikitumbuiza katika ile miaka ya 1950. Ilikuwa katika ule upigaji muziki wa Budohi ndipo alipoungana na Kawawa katika kutengenezwa kwa senama hiyo ya “Wageni Wema” ambayo mwandishi kaitaja lakini aliishia hapo tu.
Budohi na Aoko ni kati ya wafungwa wa Mau Mau waliokuwa Handeni ambako Kawawa alikuwa na jukumu la kuwaangalia. Budohi ndiyo alikuwa mtu wa kati baina ya TAA na KAU na kuanzia hali ya hatari ilipotangazwa Kenya mwaka 1952 Budohi na Aoko wakawa katika jicho kali la makachero. Makachero hawa Waafrika wanafahamika na wengine walikuja kufanya kazi hiyohiyo katika Tanganyika huru. Hiki ndicho kipindi ambacho Kaimu Rais wa TAA na Katibu wa TAA Abdulwahid Sykes alipokutana na Kenyatta Nairobi. Wakati Wakenya hawa wanafungwa Tanganyika, viongozi wa KAU akina Bildad Kaggia, Jomo Kenyatta, Kun’gu Karumba, Achieng Oneko, Paul Ngei na Fred Kubai walikuwa wamekamatwa Kenya. Kawawa ni mmoja kati ya viongozi hawa na ingependeza sana kama kupitia kwake tungeelezwa jinsi KAU na TAA ilivyokuwa ikishirikiana kwani haiwezekani kuwa Budohi na Kawawa uswahiba wao ukaishia kwenye kucheza senema tu.
Wanaharakati wote walishtushwa na kutiwa mbaroni kwa Budohi na Aoko. Haiwezekani kuwa iwe Mzee Kawawa kasahau matukio haya muhimu. Budohi na Aoko walikuwa wamefungwa minyororo walipokuwa katika selo pale Kituo cha Kati cha Polisi kwa sasa jumba hilo liko kituo cha mabasi kinachojulikana kama “station.” Waliwekwa pale kwa miezi sita muda wote wakiwa na minyororo miguuni. Waliwekwa pale kwa miezi sita wakihojiwa kabla hawajapelekwa Handeni walipomkuta Kawawa. Hivi ndivyo vitu ambavyo kwa hakika vingeongeza ladha ya kitabu cha Mzee Kawawa endapo mwandishi angechukua muda kutafiti na kuzungumza na watu waliokuwa katika harakati wakati ule ambao bado wa hai kama Ally Sykes na mdogo wake Balozi Abbas Sykes na wengine wengi ambao walikuwepo wakati ule kama Mzee Chipaka.
Katika migomo ya wakati wa kudai uhuru hakuna mgomo uliofanikiwa na kuvuta hisia za wananchi kama mgomo wa reli wa mwaka 1960 uliodumu kwa siku 62. Ukiachia kutajwa tu kama sehemu ya historia undani wake na jinsi mipango yake ilivyokwenda na nafasi ya viongozi wa Tanganyika Railway African Union (TRAU) walivyopata misaada kutoka nchi za Mashariki hivi havijawekwa wazi. Si treni, meli wala mabasi ya railway yaliyotembea kwa mieizi mitatu. Mipango ya mgomo huu ilifanyika Tabora ambako ndiko palikuwa na karakana kuu ya reli na hapo ndipo palipokuwa makao makuu ya viongozi wa TRAU, Salum Abdallah mwenyekiti na Kassanga Tumbo katibu. Kawawa ana mengi katika kadhia hii kwa kuwa yeye wakati ule ndiye alikuwa Katibu Mkuu wa TFL. Inasemekana mgomo huu miezi michache kabla Tanganyika haijapata uhuru ndiyo ilikuwa kama zinduo kwa Mwalimu Nyerere kutambua kuwa hakuwa peke yake na sauti kwa wananchi. Walikuwapo viongozi wengine pembeni yake ambao nao wakipiga wananchi wanacheza. Ilimdhihirikia kuwa huko mbeleni wanakokwenda ipo siku atapambana na viongozi hawa. Hivyo ndivyo ilivyotokea.
Inasemekana Mwalimu Nyerere akimtumia Kawawa alianza mipango kabambe ya kujitayarisha hilo lisitokee. Hii ilikuwa nukta muhimu sana kwani haukupita muda baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 viongozi hawa wa vyama vya wafanyakazi wakajikuta wamewekwa kizuizini. Wasomaji wangependa kujua Kawawa alijihisi vipi wakati viongozi wenzake wa vyama vya wafanyakazi aliofanya nao kazi wakati wa kudai uhuru wakishirikiana na TANU kama Victor Mkello, Paul Pamba, Abdallah Mwamba, Hassan Khupe, Salum Abdallah na wengine wengi walipokamatwa mwaka wa 1964 na kuwekwa kizuizini kwa amri ya Mwalimu Nyerere. Maelezo ya Mzee Kawawa katika mambo haya yangetia mwanga katika yale mengi yasiyofahamika katika historia ya Tanzania .
Waislam wangependa sana kujua hisia za Kawawa kama muumini alihisi vipi wakati makachero walipomvamia mzalendo aliyepigania uhuru wa Tanganyika Mufti wa Tanganyika Sheikh Hassan bin Amir usiku wa manane na kumrudisha Zanzibar na kuwekewa masharti kuwa hana ruhusa kurejea Tanzania Bara. Nilitegemea kusoma sakata zima la kukamatwa kwa Sheikh Hassan bin Amir na kuvunjwa kwa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) jumuia ya Waislam iliyokuwa ikipanga kujenga Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Nilitegemea halikadhalika kusoma mchango wa Mzee Kawawa katika kuunda Bakwata. Mengi yamesemwa kuhusu hujuma hii kwa Waislam moja wapo ni kuwa EAMWS ilivunjwa kwa shinikizo la Kanisa Katoliki likimtumia Mwalimu Nyerere. Hili si jambo la siri tena tafiti mbalimbali zimefanywa na vitabu kuandikwa na waandishi kutoka nje ya Tanzania kuhusu tatizo hili la kujitokeza udini mapema baada ya uhuru kupatikana. Kwa kuwa Kawawa alikuwa pamoja na Mwalimu Nyerere na alishiriki katika kuunda Bakwata wananchi hasa Waislam wangenufaika kusoma hisia zake wakati maamuzi hayo yanapitishwa na serikali. Kwa hakika kuna maamuzi mengi sana ambayo Kawawa alishiriki yaliwaumiza sana Waislam katika juhudi zao za kujitafutia elimu. Waislam wangependa sana kujua ni kipi kilikuwa kinamsukuma kufanya vile.
Kwa yeyote atakaepata bahati ya kusoma kitabu cha maisha ya Mzee Kawawa ni wazi hatakuta jipya ambalo hakuwa akilijua kabla. Kwa ajili hii basi mlango bado uko wazi kwa watafiti wengine kuandika kitabu kuhusu Rashidi Mfaume Kawawa kwani maisha ya Mzee Kawawa bado hayajaandikwa. Hata hivyo tumpongeze mwandishi kwa kazi hii kwani ni baada ya yeye kutuandikia kitabu ndipo nasi tumepata nguvu ya kunyanyua kalamu zetu na kusema.
3rd January 2010
10:44
Hapana Haja ya Kuiogopa Historia ya Uhuru wa Tanganyika
Mohamed Said
Mzee Yusuf Halimoja karudi tena safari hii anasema katika kichwa cha makala yake, “Sijasema Uhuru Uliletwa na Nyerere” (Jamhuri Januari 31 Februari 6 2012). Katika makala hii wakati mnakasha (majadilano)unanoga yeye katangaza kuwa anajitoa. Waswahili tuna msemo, “ametoa mbukwa.” Juu ya huko kujitoa madam kanitaja katika makala yake sina budi nami kumpa majibu yangu katika yale niyajuayo katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Mzee Halimoja labda kwa utu uzima huwa anasema mengi. Mimi sitajibu kila aliloandika ila nitapita mle ambamo nahisi wasomaji watafaidika na kitu kipya ambacho hawakuwa wakikijua kabla ya hapo.
Si kweli kuwa Nyerere aliongoza juhudi za uhuru peke yake. Nyerere kaja Dar es Salaam mwaka 1952 na akapokelewa na rais wa TAA Abdulwahid Sykes na alikuta mambo yako mbali sana. Kirilo kenda UNO na kurudi, TAA ishazungumza na Kamati ya Umoja wa Mataifa inayosimamia nchi zilizokuwa chini ya Udhamini na ishapeleka mapendekezo ya katiba kwa Gavana Twining, TAA imeshaunda Kamati ya Siasa na ikapeleka viongozi wake (Abbas Sykes, Japhet Kirilo na Saadan Abdu Kandoro) kutembea nchi nzima kuzungumza na wananchi kuhusu madhila ya ukoloni. Juu ya hayo yote TAA imeshafanya uhusiano na vyama vingine vya siasa kama African National Congress (ANC) ya Northern Rhodesia chini ya Kenneth Kaunda. (Ally Sykes hadi leo ana barua kadhaa alizokuwa akiandikiana na Kaunda kabla Kaunda hata hajauana na Nyerere). Vilevile Abdulwahid alikuwa kafanya mkutano na Kenyatta wakati wala Kenyatta hajasikia jina la Nyerere. Nia ya mikutano hii ilikuwa kuunganisha juhudi za TAA na KAU katika kupambana na Waingereza.
Kwa wengi mambo haya ni mageni katika masikio yao wameleweshwa na propaganda za TAA hakikuwa chama cha siasa. Simlaumu Mzee Halimoja naamini kabisa kuwa yeye haya hakuwa anayajua. Kwa Mzee Halimoja siasa Tanganyika haikuwezekana bila Nyerere na TANU chama ambacho Nyerere mwenyewe wala hana chimbuko nacho. Halimoja anazungumza kuhusu ujasiri wa Nyerere. Sawa hapana neno lakini je anaujua ujasiri wa Schneider Abdillahi Plantan katika TAA kiasi ambacho Waingereza walimkamata na kumweka kuzuizini? Je Halimoja anajua kisa cha Dome Okochi Budohi Mkenya kadi yake ya TANU na 6 kazi aliyokuwa akifanya katika harakati za TAA kabla hawajaunda TANU akiwa ndiye kiunganisho kati ya TAA na KAU ya Kenyatta? Ninaweza kumpa mifano kocho. Budohi alikamatwa mwaka 1955 pamoja na wanaharakati wengine wa Kenya kwa tuhuma za kuwa Mau Mau. Budohi alifungwa kisiwa cha Lamu kuazia 1955 hadi 1963 Kenya ilipokuwa inakaribia kupata uhuru ndipo alipoachiwa. Budohi akifahamiana vyema kabisa na wazee wangu na nimejifunza mengi kutoka kwake kuhusu TAA na TANU. Lakini kama Mzee Halimoja anataka kubaki na historia ya Nyerere inayoanza na TANU 1954 na kupuuza michango ya wengine mimi sina ugomvi na hilo. Naamini kwa haya machache msomaji kapata yale ambayo hakuwa anayajua kabla na keshatambua kuwa TAA kilikuwa chama cha siasa hata kabla Nyerere hajakutana na Abdu Sykes Dar es Salaam mwaka 1952.
Mzee Halimoja kazungumzia kuhusu Abdulwahid Sykes kuwa kwa nini natumia rejea zake. Napenda kumafahamisha kitu kimoja. Historia ya Nyerere na TANU itakuwa salama na ikafahamika kama inavyofahamika katika historia rasmi mfano wa hii ya Mzee Halimoja ikiwa tu Abdulwahid Sykes utamtoa katika historia ya TAA na TANU na historia ya Nyerere mwenyewe. Lakini pale tu utamkapomleta marehemu Abdu katika historia ya TAA na TANU itakubidi uachane na Nyerere kwanza na urudi robo karne nyuma kupata mwanzo wa harakati na hapo ndipo unapambana na Nyaraka za Sykes na hazitakuwa za Abdulwahid bali za baba yake. Hapo ndipo utakapojua umuhimu wa nyaraka hizi. Kueleza yaliyomo humo katika nyaraka hizo inataka mada itakayojitegemea yenyewe kwani ni historia inayorudi nyuma karne moja. John Iliffe aliondoka na baadhi ya nyaraka hizi ambazo alikabidhiwa na binti yake Abdu Sykes, Daisy Aisha wakati Daisy alipokuwa mwanafunzi wake wa historia miaka ya 1960 katikati Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Iliffe hajazirejesha hadi leo. Nyaraka hizo ndizo zilizomsaidia Illife kuandika historia ya TAA. Kwa nini historia ya harakati ipatikane kwa mtu mmoja tu Abdu Sykes kama anavyouliza Mzee Halimoja, jibu lake ni hili, baba yake Abdu Kleist Sykes ndiye aliyeasisi harakati za siasa Tanganyika mwaka 1929 na ameacha nyuma hazina kubwa ya maandiko. Anaetaka kujua zaidi na asome “Kleist Sykes, The Townsman” na Daisy Sykes katika “Modern Tanzania,” kitabu kilichohaririwa na John Illife.
Mzee Halimoja anasema Nyerere ndiye aliyeandika katiba ya TANU. Nataka nimweke sawa Mzee Halimoja kuhusu katiba ya TANU. Katiba ya TANU haikuandikwa na yeyote yule. Kwa ufupi ni kuwa Nyerere hakuandika katiba ya TANU. TAA Political Sub Committee ilinakili katiba ya Convention Peoples Party (CPP) ya Kwame Nkrumah neno kwa neno. Mzee Halimoja akitaka ushahidi aitafute katiba ya CPP na aifananishe na katiba ya TANU. Hilo la kwanza. Kitu cha pili napenda kumsahihisha kwa heshima zote Mzee Halimoja kuwa hiyo ilani namba 14 aliyoeleza kuwa ilitolewa na Waingereza haikuwa namba 14 bali namba tano ikijulikana kama Government Circular No. 5 (1 August 1953) ikiwakumbusha viongozi wa TAA kutojiingiza katika siasa. Haya yalitokea baada ya serikali kuwa na ushahidi kuwa TAA ilikuwa inafanya siasa dhahir shahir jambo ambalo Mzee Halimoja hataki kulisikia sharti siasa iwe na Nyerere yumo. Baada ya kuona akina Abdu Sykes na Hamza Mwapachu hawasikii wameshikilia tu kuwasakama Waingereza na serikali yao ikatoka Government Circular No.6. Hapa kuna kisa cha kuhadithia lakini kwa makala hii tutajitoa nje ya maudhui. Kipindi hiki wengi walikikimbia chama wakabaki wanamji. Abdulwahid ilibaki kidogo apoteze kazi yake kama Market Master Soko la Kariakoo. Hii ndiyo historia ya siasa ya TAA na TANU niijuayo mie, historia ambayo wazee wangu walikuwa wachezaji wa kikosi cha kwanza na wakinihadithia siku zote hadi walipotangulia mbele ya haki. Jambo la tatu Mzee Halimoja hasemi kweli kuhusu historia ya TANU katika sehemu zile ambazo kanisa lilikuwa na nguvu. Ukweli ni kuwa waliochelewa kuingia TANU si Warufiji na Wangindo bali watu wa Masasi, Peramiho na kwengineko kutokana na shinikizo la Kanisa. Niruhusu msomaji mpenzi nikudokolee kidogo mambo kutoka katika hazina ya wazee wangu.
Mkutano wa kwanza wa TANU 1955 ulihudhuriwa na Salum Mpunga na Ali Ibrahim Mnjawale kutoka Lindi. Mkutano huu ulifanyika Dar es Salaam Ukumbi wa Hindu Mandal. Baada ya mkutano, wakati wajumbe wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini. Mbali na kampeni za kuipinga TANU za Liwali Yustino Mponda ambae Mzee Halimoja anamfahamu vyema kabisa, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa Tanganyika wasijihusishe na “wafanya fujo” wanaotaka kuzusha vurugu. Twining alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi wengi kutoka sehemu za kusini kujiunga na TANU.
Mpunga na Mnjawale waliomba Nyerere aende majimbo ya kusini kuhamasisha wananchi ili wakabiliane na fitna za Gavana Twining na kampeni za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda. Ukweli ni kuwa Nyerere hakutaka kwenda katika ziara ile akijua kuwa huko alikuwa anakwenda kupambana na kanisa lake uso kwa macho. Juu hayo yote Mpunga na Mnjawale katika kikao kile walimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Katika sehemu hizo Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha safari ya Nyerere. Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.
Nyerere na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita, hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere. Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Suleiman Masudi Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.
Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.
Jumapili hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa hii maalum ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam. DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.
Wasomaji wapenzi katika makala yangu iliyopita nilimpa changamoto Mzee Halimoja aeleze ni akina nani waliingiza TANU kwao huko Masasi na Peramiho. Ukweli ni kuwa hata kugusia hili katika makala yake iliyopita hakuthubutu. Nimempa changamoto aeleze hicho anachokiita “mchango wa pekee wa Nyerere” katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Hilo vilevile limemshinda. Nashukuru kuwa kanijibu ingawa kakwepa baadhi ya mambo muhimu lakini kwa kufanya hivyo kanipa mimi nafasi ya kueleza yale ambayo naamini wengi walikuwa hawayajui. Nyerere hakuwa peke yake katika kuupigania uhuru wa Tanganyika wala hakuandika katiba ya TANU wala harakati za kupigania uhuru hakuzianzisha yeye. Nadhani haya niliyoandika yanatosha kwa sasa na ningependa kumaliza kwa kuuliza swali. Nani leo anawakumbuka wazalendo hawa nilowataja katika makala haya? Je hawastahili watu hawa kuenziwa pamoja na Nyerere?
30 Januari 2012
08:28
MATUNDU KATIKA HISTORIA YA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA
MATUNDU KATIKA HISTORIA YA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA
Mohamed Said
Wakati marehemu Abdulwahid Sykes[1]akiwa katika harakati za uongozi wa TAA alikuwa akifanya kazi kama Market Master soko la Kariakoo. Ofisi yake ilikuwa kati ya Mtaa wa Swahili mbele Mtaa wa Mkunguni na nyuma yake Mtaa wa Tandamti. Mtaa huu wa Tandamti umebadilishwa jina sasa unajulikana kama Mshume Kiyate ingawa wahusika hawajabadili kibao sasa takriban miaka kumi na zaidi kwa kuwa wanapinga mabadiliko hayo kwa fikra kuwa kilichopelekea Meya wa Dar es Salaam Kitwana Selemani Kondo kumuenzi Mshume Kiyate ni udini na wala si uzalendo na mchango wa muhusika katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Huenda kizazi cha leo na wanasiasa wa sasa hawawajui mashujaa wa nchi yetu na yaliyokuwa yakipitika pale Kariakoo ofisini kwa Abdulwahid.
Katika ofisi ile alikuwapo Mzee Abdallah yeye alikuwa ndiyo mhudumu wa ofisi na alimjua Mwalimu Nyerere pale ofisini kwa Abdulwahid na anachokumbuka kwa maskhara ni ile kazi yake ya kuchukua kuku pale sokoni akawachinja na kumpelekea Mama Daisy, mke wa Abdulwahid kwa ajili ya chakula cha mchana cha Nyerere na wanaharakati wengine hasa Nyerere alipoacha kazi ya ualimu na kuja kukaa na Abdulwahid kwa muda kabla hajenda Musoma. Pale ndipo ilipokuwa sehemu kuu ya mawasiliano ya TAA. Wakati ule Abdulwahid alikuwa katibu wa TAA na Dr. Vedasto Kyaruzi alikuwa ndiye rais.
Wakati ulikuwa miaka ya mwanzo 1950 na Abdulwahid Sykes alikuwa keshakutana na Jomo Kenyatta Nairobi na kufanya mkutano na KAU nia ikiwa ni kuunganisha nguvu za TAA na KAU yaani juhudi za Watanganyika na Wakenya kupambana na ukoloni. Harakati hizi zilipelekea kuwa na mawasiliano ya karibu sana na ya siri kati ya Abdulwahid Sykes na Kenyatta kiasi kwamba mwaka 1953 Kenyatta alimwalika kwa mara ya pili Abdulwahid Nairobi katika mkutano mwingine ambao alikuwa aende na Dossa Aziz. Ule mkutano wa kwanza Abdulwahid alisindikizwa mkutanoni na Ahmed Rashad Ali ambae baadae alikuja kuwa mtangazaji maarufu wa Radio ya Ukombozi wa Africa (Radio Free Africa) kutoka Cairo . Kutokana na mkutano huu Rashad akaja fahamiana vizuri sana na Kenyatta. Kipindi hiki harakati dhidi ya ukoloni zilikuwa zimepamba moto Afrika.
Kipindi hiki cha miaka ya mwanzo wa 1950 TAA ilikuwa kama vile inatoka usingizini na kuanza kufanya siasa za kweli chini ya uongozi wa vijana baada ya kuuangusha uongozi uliopita uliokuwa umehodhiwa na wazee waliosomeshwa na utawala wa Kijerumani rais wa TAA akiwa Mwalimu Thomas Plantan na katibu wake Clement Mtamila. Abdulwahid na Ally Sykes walikuwa na mawasiliano na Kenneth David Kaunda katibu wa African National Congress pamoja na Asia Socialist Conference Anti-Colonial Bureau. Idara ya Usalama ya kikoloni ikijulikana kama Special Branch walikuwa wakifuatilia kwa karibu sana nyendo za ndugu hawa. Mtafiti akipitia nyaraka za Sykes atakutana na shajara za marehemu Abdulwahid baadhi zikiwa zimeandikwa kwa hati ya kawaida na nyingine zikiwa katika hati mkato. Inaaminika shajara zake za hati mkato ndizo zenye taarifa nyingi za harakati zake za kuanzisha TANU na safari zake nje ya nchi kukutana na wapigania uhuru wengine kama Jomo Kenyatta, Bildad Kaggia, Kung’u Karumba, Achieng Oneko, Fred Kubai na Paul Ngei. Hawa walikuja fahamika kama “Kapenguria Six” kwa kuwa walifungwa jela kwa tuhuma za Mau Mau sehemu hiyo inayojulikana kama Kapenguria.
Bahati mbaya ni kuwa akina Sykes wenyewe hawajaruhusu watafiti kuzisoma shajara za marehemu Abdulwahid ambazo sasa takriban zina umri wa zaidi ya miaka hamsini. Nyaraka za siri za serikali ya kikoloni ambazo sasa ziko wazi huko Uingereza baada ya kupita miaka hamsini zinaonyesha kuwa Abdulwahid wakati akiwa mfanyakazi wa Soko la Kariakoo nyendo zake zilikuwa zikifuatiliwa kwa karibu sana na “Special Branch” kiasi cha kuwa jalada lake la siri limemtaja kama “mtu hatari.” Katika halmashauri ya TAA walikuwapo Waafrika kutoka Kenya na Nyasaland kama Dome Okochi Budohi na Patrick Aoko kutoka Kenya na Denis Phombeah kutoka Nyasaland wakiendesha harakati bega kwa bega na ndugu zao Watanganyika.
Wakati akina Bildad Kaggia na Kenyatta lile kundi la Kapenguria likikamatwa Nairobi baada ya muda Budohi na Aoko nao walitiwa mbaroni Dar es Salaam . Abdulwahid ilibidi akaimu nafasi ya rais baada ya Dr. Kyaruzi kupewa uhamisho kwenda Kingolwira kama adhabu ya kupinga serikali. Kama kuna mtu ana fikra kuwa TAA haikuanzishwa kwa ajili ya kudai uhuru wa Tanganyika basi na aeleze hizi harakati za viongozi wake kuweka mikakati ya pamoja na akina Jomo Kenyatta na Kenneth Kaunda katikati ya 1950 na 1953 na kuweka uhusiano na vyombo kama Asia Socialist Anti- Colonial Bureau ilikuwa ya kutafuta nini. Vilevile aeleze kwa nini serikali ilitoa sekula no. 5 na 6 ikiwaonya Waafrika watumishi wa serikali kuhusu kufanya siasa wakiwa watumishi wa Malkia.
Mwalimu Nyerere na Abdulwahid walikujafahamiana mwaka 1952 na Nyerere alipelekwa nyumbani kwa Abdulwahid na Joseph Kasella Bantu. Nyerere alikuwa akija mjini lazima atapita ofisini kwa Abdulwahid Sykes pale sokoni Kariakoo ikiwa siku za kazi. Siku za Jumapili alikuwa akienda Mtaa wa Mbaruku nyumbani kwa Dossa.
Siku zile akiwa pale kwa Abdulwahid akenda ofisini kwake Kariakoo na wakati wa chakula cha mchana Mwalimu Nyerere alikuwa akiongozana na Shariff Attas ambae alikuwa akifanya kazi chini ya Abdulwahid Sykes kama dalali wa soko. Shariff Attas alikuwa akiongozana na Nyerere kwenda nyumbani kwa Abdulwahid kwa ajili ya chakula. Jambo hili likawafanya Shariff Attas na Mwalimu Nyerere wawe karibu sana na wajuane vizuri. Nyumba ya Abdulwahid Sykes haikuwa mbali sana na soko, ilikuwa Mtaa wa Aggrey na Sikukuu nyumba ya kona. Shariff Attas na Mama Daisy ni mmoja wa watu wa mwanzo kujuana na Mwalimu Nyerere achilia mbali kuwa walikuja kuwa wanachama wa mwanzo wa TANU ilipokuja kuundwa mwaka 1954. Mwalimu Nyerere alipokuja Dar es Salaam na mkewe Mama Maria, Mama Daisy ndiye aliyempokea Mama Maria na kumtoa ukumbi.
Kupitia kwa Abdulwahid Sykes Mwalimu Nyerere akajuana na watu wengine pale sokoni mashuhuri mjini kama Mshume Kiyate, Shariff Mbayamtu na wengineo. Mshume Kiyate akampenda Mwalimu Nyerere kama mwanae. Wakati wa kudai uhuru baina ya 1954 hadi 1961 Mzee Mshume alijitolea kuiangalia na kuitunza familia ya Mwalimu Nyerere ili Nyerere ashughulike na TANU tu asihangaike na adha ya kuhemea chakula cha wanae. Mzee Mshume na Mwalimu Nyerere wote wawili walikuwa wapenzi wa kucheza bao na wakati mwingine Mzee Mshume akicheza bao na Mama Maria. Ofisi ya Abdulwahid pale Kariakoo na ofisi ya Hamza Mwapachu[2]Ilala Wefare Centre ndipo palipokuwa na pilikapilika za ingia toka za wanasiasa wa wakati ule kwa nyakati za mchana na ikiingia usiku harakati zilihamia Tanga Club iliyokuwa Mtaa wa New Street na Mkunguni.
Uchaguzi wa rais wa TAA wa 1953 kati ya Abdulwahid Sykes aliekuwa akitetea kiti chake na Julius Nyerere ulikuwa uchaguzi wa aina yake katika historia ya uhuru wa Tanganyika . Ulitanguliwa na majadiliano ndani ya Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA kueleza umuhimu wa kumweka Nyerere katika kiti badala ya Abdulwahid ambae muda wake wa uongozi ulikuwa unakwisha. Hapa ndipo mwanzo wa matundu na chanzo cha matatizo ya historia ya kudai uhuru wa Tanganyika . Kwa kuwa Nyerere mwenyewe hakupata kueleza vipi aliingia TANU inaonekana kama alizuka tu kutoka Musoma akatua Dar es Salaam na kuanzisha TANU. Jambo ambalo haliwezekani.
Ukweli wa mambo ni kuwa uchaguzi baina rais wa TAA, Abdulwahid Julius Nyerere, ulifanyika kwenye Ukumbi wa Arnatouglo tarehe 17 Aprili, 1953. Nje ya uongozi wa TAA ambao ulimpendekeza kugombea nafasi hiyo, Nyerere alikuwa mgeni kabisa kwa wote aliokuwa akiwaomba kura zao. Nyerere alikuwa mgeni na alikuwa hana historia ya kuongoza mapambano ya umma dhidi ya serikali ya kikoloni. Ukoo wa Sykes ulikuwa maarufu na unatambulikana katika siasa za Dar es Salaam kwa takriban robo karne. Ushahidi wa haya unapatikana katika nyaraka kati ya ukoo huu na serikali ya kikoloni. Katika kipindi cha miaka zaidi ya ishirini, serikali kwa nyakati tofauti, kati ya mwaka 1929 hadi 1953 ilikuwa na barua za Kleist Sykes [3] na za mwanaye Abdulwahid wakiwa viongozi wa African Association wakichagiza serikali kuhusu madhila tofauti yaliyokuwa yakiwakabili wananchi. Maarufu katika hayo ni migomo ya wafanyakazi kati ya mwaka wa 1938 hadi 1947 na ule mgogoro wa ardhi ya Wameru.
Uchaguzi ulikuwa kwa kunyoosha mikono. Denis Phombeah[4] aliyekuwa akifanya kazi Ukumbi wa Arnatouglo ndiye alikuwa msimamizi wa uchaguzi. Phombeah aliwaomba Abdulwahid na Nyerere kutoka nje ya ukumbi ili uchaguzi uanze. Wiki nzima kabla ya uchaguzi Phombeah alikuwa akizunguka mji mzima na pikipiki yake akimfanyia kampeni Nyerere. Lakini kwa hakika hakukuwa na haja ya kufanya hivyo. Uongozi wa ndani wa TAA wa Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz na John Rupia ulikuwa tayari umekwishaamua kumpa Nyerere urais wa chama. Uchaguzi ulikuwa kutimiza utaratibu tu. Baada ya Abdulwahid na Nyerere kuombwa na Phombeah kutoka nje, upigaji kura ulianza.
Nyerere alishinda uchaguzi huo dhidi ya Abdulwahid kwa kura chache sana. Huu ulikuwa ndiyo mwanzo wa Nyerere kujulikana katika siasa za Tanganyika. Kuanzia siku ile historia ya Tanganyika ikabadilika na siasa za Tanganyika zikachukua sura nyingine kabisa. Siasa zilichukua sura nyingine kwa sababu walingia watu katika harakati ambao waligeuza mwelekeo kudai haki kwa vipaji vya kuhamasisha watu ambavyo Tanganyika ilikuwa haijapata kuona. Hapa ndipo unapokutana na Titi Mohamed,[5] Tatu bint Mzee, Said Chamwenyewe,[6] Sheikh Suleiman Takadir,[7] na wengine wengi lakini kwa bahati mbaya hawa wote historia imewasahau hawatajwi kabisa.
Nyerere mwenyewe kamwe hajazungumzia kuhusu uchaguzi huu au namna alivyokuja kuongoza TAA Dar es Salaam. Kiasi cha karibu sana alichofika kumhusisha Abdulwahid na historia yake kilikuwa katika ile hotuba ya mwaka wa 1985 ya kuwaaga wazee Dar es Salaam, na kwa bahati mbaya Nyerere alipojaribu kumueleza Abdulwahid, alishindwa kwa kuwa kwa kauli yake alisema hakumbuki cheo alichokuwa akishika Abdulwahid katika TAA wakati yeye Nyerere alipojiunga na chama mwaka 1952. Hata hivyo gazeti la serikali, “Daily News” lilijaribu kurekebisha historia kwa kutaja cheo cha Abdulwahid, ingawa kwa makosa, kwa kusema kuwa Nyerere alipojiunga na TAA makao makuu Abdulwahid alikuwa katibu. Ukweli ni kuwa Nyerere alimkuta Abdulwahid akiwa rais wa TAA. Nini sababu ya mparaganyiko huu?
Kleist Sykes baba yao Abdulwahid, Ally na Abbas ameacha kumbukumbu nyingi zinazoelezea si tu hali ya siasa Tanganyika ilivyokuwa mwanzo wa karne ya ishirini bali zinatoa historia kamili ya mji wa Dar es Salaam na watu wake na jinsi yeye mwenyewe alivyoasisi African Association. Ukipitia nyaraka hizo zinakurudisha miaka mia moja nyuma toka baba yake Kleist, Sykes Mbuwani alipoingia nchini Tanganyika kama mamluki akiwa katika jeshi la Wazulu mia nne wakiongozwa na Mjerumani Von Wissman kuja kupigana na Bushiri bin Salim Pangani na Chifu Mkwawa huko Kalenga. Nyaraka zinaonyesha maisha ya Kleist katika jeshi la Wajerumani katika Vita Kuu ya Kwanza akiwa Aide de Camp (Mpambe) wa Von Lettow Vorbeck. Nyaraka zinafichua vipi Kleist alikuja kuwa mwanasiasa hodari na kiongozi wa chama cha wafanyakazi katika kipindi cha vita kuu mbili za dunia baada ya kukutana na Dr James Kwegyir Aggrey mwaka 1924 na kumshauri aanzishe umoja wa Waafrika katika Tanganyika.
Kutokana na ushauri huu wa Dr Aggrey mwaka wa 1929 Kleist na baadhi ya rafiki zake wa karibu kama Mzee bin Sudi, ambaye wazazi wake walikuwa Wamanyema kutoka Belgian Congo, Ibrahim Hamis - Mnubi ambaye baba yake alitoka Daffur nchini Sudan, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima - Mzaramo, Suleiman Majisu, Raikes Kusi, Rawson Watts na Cecil Matola - Myao kutoka Masasi walianzisha African Association, Kleist akiwa katibu muasisi. Gavana wa wakati ule Donald Cameroon akawaonya akina Kleist kuwa wasikiingize chama katika siasa. Mikutano ya mwanzo ya chama hiki ilifanyika Mtaa wa Masasi Mission Quarter Dar es Salaam kwenye nyumba ambayo ilikuja hapo baadae ikanunuliwa na John Rupia. Mwaka wa 1930 katika juhudi za kuikiimarisha chama, Kleist akawa anasimamia ujenzi wa jengo la makao makuu ya African Association, New Street (sasa Mtaa wa Lumumba) ambalo wananchi walikuwa wakijenga ofisi yao hiyo kwa kujitolea nguvu zao wenyewe. Hili ndilo jengo ambalo TANU ilikuja kuzaliwa tarehe 7 Julai, 1954.
Wakristo walionywa na wamisionari wasijihusishe na African Association kwa kuwa harakati zao ni kupinga serikali. Haya yote ameyaeleza Kleist katika kumbukumbu zake alizoacha kabla ya kifo chake mwaka 1949. Abdulwahid akiwa mtoto mdogo alipata kueleza kuwa ameshuhudia kwa macho yake ujenzi wa jengo la TAA kwa kuwa alikuwa akifuatana na baba yake pale New Street siku za Jumapili ambayo ndiyo ilikuwa siku ya ujenzi. Kleist hakuishia hapo baada ya kuasisi African Association mwaka 1929 akaasisi “Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ” (Umoja wa Waislam wa Tanganyika ) mwaka 1933 akiwa katibu. Vyama hivi viwili vikawa vinafanya kazi kwa pamoja kwa kuwa viongozi hao hao wa TAA ndiyo wakajakuwa viongozi wa “Al Jamiatul Islamiyya” na huu ndiyo ulikuwa mtindo hadi mwaka wa 1954 TANU ilipoasisiwa. Mweka Hazina wa “Al Jamiatul Islamiyya” Iddi Faizi Mafongo[8]ndiye aliyekuwa pia mweka hazina wa TANU na “Al Jamiatul Islamiyya” ilitoa fedha katika kuchangia safari ya Nyerere Umoja wa Mataifa mwaka 1955.
Watu wengi hawajui kuwa ile hotuba aliyosoma Nyerere Umoja wa Mataifa iliandikwa mwaka 1950 na Kamati Ndogo ya Siasa ndani ya TAA iliyoasisiwa na Abdulwahid Sykes wajumbe wake wakiwa Sheikh Hassan bin Amir kama mufti wa Tanganyika na Zanzibar ; Dr Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, Said Chaurembo aliyekuwa liwali wa mahakama ya Kariakoo; John Rupia na Stephen Mhando.[9] Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kushughulika na masuala yote ya siasa katika Tanganyika. Kuundwa kwake ndiyo hasa ulikuwa mwanzo wa siasa za dhahiri katika Tanganyika na mwanzo wa harakati za kudai uhuru wa Mtanganyika.
Inasikitisha kuwa Mwalimu Nyerere hakupata kueleza chanzo cha hotuba ile ambayo hivi sasa imo katika moja ya vitabu vyake na kwa hakika hiki ni kisa kirefu sana na cha kumvutia mtafiti yeyote. Waraka huu ulokuwa chanzo cha hotuba ya Mwalimu Nyerere Umoja wa Mataifa umepotea na haujulikani ulipo. Jalada lake Tanzania National Archive (TNA) ni tupu na hata “microfilm” ya waraka ule imetoweka. Laiti ungelipatikana mtafiti angeliona sahihi ya marehemu Abdulwahid Sykes, Vedasto Kyaruzi, Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu na wajumbe wengine. Mtafiti akitaka kujua vipi African Association iliasisiwa na ni nani wahusika wakuu basi hana budi kusoma nyaraka za Kleist Sykes lakini ikiwa atataka kutafiti kuhusu TANU itabidi asome nyaraka pamoja na shajara za Abdulwahid Sykes.
Ikiwa huu ndiyo ukweli wa historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika huu ubishi wa kuwa nani kaasisi TAA umetoka wapi? Halikadhlika unaweza mtu ukahoji kwa nini waliokuja baada ya TAA waseme kuwa hapa ndipo ilipozaliwa TANU badala ya kusema kuwa hapa ndipo ilipozaliwa TAA? Au vipi ikawa muhali kunasibisha familia ya Kleist Sykes na nguvu ya Watanganyika kujikomboa? Kipi kinachoogopwa? [10] Hivi kweli Nyerere angeweza kuukana ukweli huu mbele ya watu wa kawaida tu na wala si wanasisasa, watu kama Shariff Attas na Mzee Abdallah na akabaki na heshima yake achilia mbali wanasiasa wa wakati ule kama Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu, Dr. Kyaruzi na wengineo?
Ama kuenezwa kwa TANU katika majimbo hiyo kazi ilifanywa na wengi ambao leo hawatajwi na hata pale Mwalimu Nyerere alipotoa medali 3979 mwaka wa 1985 katika viwanja vya Ikulu kwa Watanzania waliofanya mengi katika nchi hiii ilistaajabisha wengi kuwa hakuna hata mmoja wa waliopigania uhuru aliyepata heshima hiyo. Si Dossa Aziz, wala Abdulwahid Sykes au Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Yusuf Badi, Tatu bint Mzee, Mshume Kiyate, Mwinjuma Mwinyikambi, Suleiman Masudi Mnonji, Bi. Shariffa Mzee, Sheikh Mohamed Ramia, Zuberi Mtemvu, Ali Mwinyi Tambwe, Hamza Mwapachu, Dr. Kyaruzi, Dr. Michael Lugazia, Ali Migeyo,[11]Suedi Kagasheki, Iddi Faiz Mafongo, Yusuf Olotu, Yusuf Chembera, Salum Mpunga,[12]Hamisi Taratibu, Omari Suleiman,[13]John Rupia, Joseph Kasella Bantu [14]na wengine wengi. Hakuna katika mashujaa wa uhuru aliekumbukwa kwa kupewa medali licha ya kuwa wao walitembea nchi nzima kuieneza TANU pamoja na Nyerere.
Wala si kweli kuwa wazalendo hawa hawakumaliza kazi. Abdulwahid na Ally Sykes walifadhili chama hadi uhuru unapatikana. Inatosha kusema tu Dossa Aziz alifadhili chama hadi kufikia kufilisika kabisa na akafa kijijini Mlandizi akiwa masikini kabisa. Sheikh Hassan bin Amir katika kumbukumbu zake anasema alijiuzulu siasa baada ya uhuru kupatikana na kuanzisha Daawat Islamiyya ili ashughulikie elimu kwa Waislam na hii ndiyo ikawa kisa cha ugomvi baina yake na Nyerere mwishowe Mufti Sheikh Hassan bin Amir akakamatwa kwa amri ya Nyerere na kurejeshwa kwao Zanzibar. Baraza la Wazee wa TANU lilikokuwa na wajumbe 170 wote Waislam chini ya uenyekiti wa Iddi Tulio baada ya kufukuzwa Sheikh Takadir TANU lilishiriki katika mapambano hadi mwisho na lilikuja kuvunjwa na Nyerere mwaka 1963 kwa madai ati wazee wale wa Kiislamu walikuwa wakichanganya dini na siasa. Ama kuhusu Waislam na Nyerere kuhusu udini hili ni somo tosha linalohitaji muda wa pekee. Na ni katika huo udini ndipo iNakapojitokeza leo kwa nini Waislam hawamwiti tena Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa bali wanamwita Baba wa Kanisa.
Mwalimu Nyerere alitaka historia ya TANU iandikwe na fikra hii ilitokea katika mjadala ulofanyika kati yake Abdulwahid, Mwalimu Kihere na Dossa Aziz. Mwalimu alimpa kazi hiyo ya uandishi wa historia ya kudai uhuru wa Tanganyika Abdulwahid Nyerere akamteua Dr. Wibert Kleruu awe msaidizi wa Abdulwahid katika kazi ile. Hii ilikuwa baada ya uhuru kupatikana. Historia iliandikwa lakini Nyerere inasemekana alisononeshwa sana na mchango wa familia ya Sykes katika siasa za Tanganyika. Historia ya Sykes Mbuwane na Von Wissman wakati wa enzi wa utawala wa Wajerumani kisha historia ya Kleist Sykes na Von Lettow Vorbeck wakati wa Wajerumani na kuingia utawala wa Waingereza ilikuwa mithili ya mchezo mzuri wa senema kutoka Hollywood. Historia yake binafsi Abdulwahid kuanzia Burma hadi kurejea Tanganyika na harakati zake na akina Kenyatta, Japhet Kirilo [15]na Earl Seaton hadi kufikia Kirilo na Seaton kwenda Umoja wa Mataifa mwaka 1952 iliingiza husda katika moyo wa Nyerere. Husda kama ijulikanavyo ni maradhi yasiyo na tiba.
Historia ile ilimwonyesha baba yake Abdulwahid Mzee Kleist kama Mwafrika alielimika vizuri kwa viwango vya wakati ule. Kleist akizungumza Kijerumani na Kiingereza, akijua kupiga chapa na hati mkato. Kleist alikuwa mwanasiasa wa kuheshimika na aliasisi chombo ambacho ndicho kulichokuja kuasisi TANU. Kleist alikuja kuwa mfanyabiashara na akatajirika. Halikadhalika historia ya mwanae Abdulwahid ilikuwa ya kupendeza iliyojaa matokeo mengi yaliyoendana na historia ya Afrika baada ya Vita Kuu ya Pili. Akiwa katika kikosi cha askari wa miguu huko Burma historia ilionyesha kuwa Abdulwahid alionyesha fikra za kutaka kuwaunganisha Watanganyika chini ya TANU. Fikra hii aliitoa siku ya mkesha wa Krismas mwaka 1945 akiwa Kalieni Camp India pamoja na askari wenzake wakingojea meli kurudi Tanganyika baada ya kwisha vita.
Aliporudi Tanganyika Abdulwahid aliendeleza harakati akiwa katibu wa Dockworkers Union mwaka 1948 hadi alipochukua uongozi wa TAA mwaka 1950 baada ya kifo cha baba yake mwaka 1949. Nyerere akisoma yale aliyokuwa akiandika Abdulwahid alifahamu kuwa kabla ya yeye kushika nafasi ya urais wa TAA nafasi ile Abdulwahid alimuomba Chifu Kidaha Makwaia aichuke lakini Kidaha hakutaka. Hakika maisha yote ya Abdulwahid yalijaa matokeo na visa vya kutosha kuandika kitabu cha historia. Chifu Kidaha na Nyerere walikuja wakawa mahasimu wakubwa na Chifu Kidaha akahamia Kenya .
Inasemekana Nyerere alipokuwa akisioma habari hizi za ukoo wa Sykes ndipo alipomjua kwa undani marehemu Abdulwahid na alijihisi kupwaya katika historia ile. Kweli baba yake alikuwa Chifu wa Wazanaki lakini hakuwa na historia yoyote ambayo angewezanae kuieleza mbele ya watu na watu wakamsikiliza. Hakuna aliyemjua baba yake Nyerere wala hata kama alipata elimu. Abduwahid alikuwa na nyaraka na taarifa za histioria ya wazee wake zilizokwenda nyuma miaka mia moja. Kuanzia Mozambique Kwa Likunyi alipotoka babu yake ambae alikuwa shemeji wa Chifu Mohosh wa Wazulu hadi walipoingia Tanganyika miaka ya mwisho ya 1800 na mchango wao katika kulipigania taifa dhidi ya ukoloni. Historia hii Nyerere aliikataa na kwa hakika ikakatalika hadi leo. Ndiyo maana imefika hadi inakatalika kunasibisha harakati za uhuru na familia ya akina Sykes. Waswahili tuna msemo “Penye ukweli uongo hujitenga.”
Abdulwahid alipotambua kuwa Nyerere hakuwa na nia hasa ya kutafiti na kuandika historia ya kweli ya Tanganyika haraka akajitoa katika kazi ile. Kazi hii alikuwa akiifanyia katika ofisi za TANU ofisi ile ile ambayo aliitumia wakati akiwa rais wa TAA. Inasemekana baada ya hapo Abdulwahid hakukanyaga tena ofisi ya TANU hadi mauti yalipomfika mwaka wa 1968. Lakini kubwa zaidi ni kuwa aliuzuia ulimi wake kusema chochote kuhusu TANU na mchango wake. Hata Lady Judith Listowel [16]aliyeandika “The Making of Tanganyika” alipokuja Tanganyika kufanya utafiti, Abdulwahid hakufungua kifua chake. Hata hivyo Dr Kleruu aliendelea na utafiti na akakamilisha historia ya TANU. Haijulikani mswada wa Klerru uko wapi lakini waliousoma wanasema umefuta mchango mzima wa marehemu Abdulwahid Sykes na mchango mzima wa Waislam katika kuunda TAA na baadae TANU katika kupigania uhuru wa Tanganyika.[17]
Baada ya kupatikana uhuru mwaka 1961 iko siku Mwalimu Nyerere alikwenda ofisi ya TANU. Pale akamkuta Shariff Attas. Mwalimu alimwuliza Shariff Attas wapi wamekutana kwani sura yake inaonyesha kama wanafahamiana. Shariff Attas kwa utulivu akamjibu Nyerere kuwa hawajapata kukutana katika maisha yao. Shariff Attas alikuwa kidogo ameghadhibika akiona kama vile sasa Nyerere kawa rais wa nchi kesha wasahau rafiki zake wa zamani na yeye hakuwa tayari kujipendekeza kwake akamwambia kwa mkato kuwa hawajuani. Lakini kubwa zaidi na la kushangaza ni kuwa Nyerere mwaka 1985 katika hotuba ya kuwaaga wazee wa Dar es Salaam aliokuwanao wakati wa kupigania uhuru alisema kuwa katika vijana waliokuwepo wakati ule alikuwa Dossa Aziz na Abdul Sykes lakini hakumbuki Abdulwahid alikuwa na cheo gani katika TAA.
Inasemekana katika kipindi chake chote alipokuwa madarakani Nyerere hakupata kusikika kuwataja katika hadhira yoyote viongozi wa TAA aliowakuta katika siasa kabla yake. Watu kama Dr. Vedasto Kyaruzi,[18] Dr. Luciano Tsere, Dr. Joseph Mutahangalwa, Dr. Michael Lugazia, Dr. Wilbard Mwanjisi[19] na wengineo. Historia ya harakati za uhuru wa Tanganyika inalazimishwa ianze na Nyerere kiasi kwamba inapotajwa kuwa Nyerere alichukua uongozi wa TAA mwaka 1953 haitajwi kauchukua uongozi huo kwa nani na katika mazingira gani. Inawezekana kweli mtu wa kiwango cha akili ya Mwalimu Nyerere akawa na kumbukumbu fupi kiasi cha kusahau kuwa aligombea nafasi ya urais wa TANU na Abdulwahid Sykes? Siku alipojaribu kumtaja Abdulwahid Sykes ndipo ulimi ukamteleza akasema hakumbuki Abdulwahid Sykes alikuwa na cheo gani katika TAA. Jambo la kusikitisha ni kuwa aliyasema maneno hayo mbele ya wazee wa Dar es Salaam ambao yeye asingewajua sama na Abdulwahid na Dossa. Leo hii si tabu kujua picha aloiacha Mwalimu Nyerere kwa wazee wale. Ilikuwa Nyerere kafika safari yake lakini kasahau kituo alichopandia basi.
Kweli inawezekana vipi Nyerere akawa kasahau uchaguzi ambao ndiyo uliomwingiza yeye katika siasa na uongozi wa Waafrika wa Tanganyika na mwishowe kuupata ubaba wa taifa? Nyerere anaweza kweli kamsahau Shariff Attas dalali wa soko au hata Mzee Abdallah muhudumu wa ofisi ya Abdulwahid lakini vipi Nyerere amsahau rafiki yake Abdulwahid mtu aliempokea Dar es Salaam akaishi nyumbani kwake alipoacha kazi, mtu alieshughulika na safari yake ya kwenda Umoja wa Mataifa kwa niaba ya TANU na mtu aliyemwingiza na kumpa uongozi wa TAA na kumkabidhi majalada na ofisi ya chama achilia mbali ile kumjulisha kwa wanachama na watu mashuhuri wa mjini?
Mwandishi wa makala haya alipoandika kitabu kuhusu maisha ya Abdulwahid Sykes “The Life and Times of Abduwahid Sykes (1924 – 1968) the Untold Story of the Muslim Struggle against British Colonialism in Tanganyika” alimlaumu John Illife ambae aliandika sana kuhusu historia ya Tanganyika kwa kutokuwa makini katika utafiti wake kiasi cha kukosa kuzisoma nyaraka za Sykes na hivyo kuandika historia iliyokuwa na ukweli nusu. John Iliffe alipoandika pitio la kitabu katika Cambridge Journal of African History aliandika kwa hasira na kusema kuwa Abduwahid Sykes hakuasisi TANU. Hata hivyo Jonathan Glassman na James Brenan wanahistoria vijana na mahiri katika historia ya Tanganyika wamesema kuwa si rahisi kwa mtafiti yeyote kupuuza kitabu hicho kwani kimekuja na mengi mapya ambayo hayakuwa yanafahamika kwa wengi.
Kwa kumalizia ningependa kusema kuwa isidhaniwe kuwa kwa kuwapuuza wazalendo wengine na kubadilisha historia ndipo ilipo njia ya kumjenga Nyerere. Kwa kufanya hivyo hawamjengi bali wanambomoa vibaya sana hasa ikiwa sasa Mwalimu Nyerere yuko katika mchakato wa kuwa “mwenye heri” kuelekea kuwa “mtakatifu” kamili. Uongo na udanganyifu si sifa ya utakatifu. Itapendeza ikiwa tutamuenzi Mwalimu kwa yale anayostahili na yapo mengi sana.
21 December 2009
[1] Habari kamili za Abdulwahid Sykes angalia Mohamed Said Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati za Waislam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza,Phoenix Publishers, Nairobi 2002.
[2] Hamza Mwapachu Mdigo kutoka Tanga ndiyo aliyemtambulisha Julius Nyerere kwa Abdulwabid Sykes. Mwapachu allikuwa kati ya waanasiasa wa mwazo wa mrengo wa kushoto na alikuwa na mafungamano na wanaharakati Wazungu katika Labour Party ya Uingereza ambao walikuwa na msimamo mkali dhidi ya ukoloni. Mwapachu alifariki mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 44.
[3] Kuhusu maisha ya Kleist Sykes soma Daisy Sykes Buruku, Kleist Sykes The Townsman katika, Modern Tanzanians, Illife, John (ed), East African Publishing House, Nairobi, 1973.
[4] Denis Phombeah aligombana na Nyerere baada ya uhuru na mwisho akakimbia nchi.
[5] Titi Mohamed alianza kuhutubia mikutano ya TANU katika viwanja vya Mnazi Mmoja kabla hajamjua Julius Nyerere aliingizwa TANU na Schneider Plantan.
[6] Said Chamwenyewe ndiye liyeitafutia TANU wanachama wa mwanzo kutoka Rufiji alikotumwa na Abdulwahid Sykes Julai 1954. Alitoka TANU baada ya kuhitilafiana na Nyerere kuhusu Kura Tatu akamuunga mkono Zuberi Mtemvu katika African National Congress.
[7] Sheikh Suleiman Takadir alifukuzwa TANU kwa kumshutumu Nyerere kuwa uhuru ukipatikana hatawatendea haki Waislam walioupigania uhuru wa Tanganyika. Sheikh Takadir ndiye aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU Dar es Salaam.
[8] Iddi Faizi Mafongo na ndugu yake Iddi Tosiri ndiyo waliompeleka Nyerere Bagamoyo Kumtambulisha kwa ndugu yao Sheikh Mohamed Ramia Khalifa wa Tariqa Kadiriyya. Sheikh Ramia na Nyerere wakaja kuwa marafiki wakubwa sana. Iddi Faizi Mafongo ndiye aliyetumwa Tanga na TANU kwenda kuchukua fedha kutoka kwa Mwalimu Kihere kuja kukamilisha nauli ya Nyerere kwa safari ya Umoja wa Mataifa mwaka wa 1955. Special Branch walimkamata njiani Turiani wakamshusha kwenye basi lakini hawakuziona fedha zile na zikafika Dar es Salaam ofisi ya TANU salama.
[9] Mwalimu Stephen Mhando alikataa kufundisha wanafunzi wake kwa mtaaala wa kikoloni na kila alipopata nafasi aliwasomesha wanafunzi wake historia ya kweli ya uzalendo na ushujaa wa Mwafrika. Aligoma kabisa kuwaita Susi na Chuma waliobeba mwili wa David Livingstone kuwa walikuwa watumishi. Yeye aliwaitikadi kuwa walikuwa rafiki wa David Livingstone. Mwalimu Stephen Mhando alikuwa bingwa wa lugha ya Kiingereza na ni mmoja pamoja na Abdwahid Sykes, Hamza Mwapachu, Dr. Vedasto Kyaruzi, Sheikh Hassan bin Amir katika wanakamati wa TAA walioandika Memorundum iliyopelekwa kwa Gavana Edward Twinning mwaka 1949 na hiyo memorandum ikaja kuwa msingi wa hotuba ya Julius Nyerere Umoja wa Mataifa mwaka 1955. Kwa habari zaidi angalia Cranford Pratt, Cranford Pratt, The Critical Phase in Tanzania 1945-1968,Cambridge University Press, London, 1976, uk. 29-31.
[10] Mara ya kwanza kuchapwa historia kinzani na historia rasmi ya uhuru wa Tanganyika ilikuwa mwaka wa 1988. Angalia Mohamed Said, ‘In Praise of Ancestors’ Africa Events,London, March/April 1988, uk. 37-41. Kada wa Chama Cha Mapinduzi akiandika kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma alitoa vitisho kwa mwandishi. Angalia Africa Events, May, 1988, barua ya Dr. K. Mayanja Kiwanuka.
[11] Soma maisha ya Ali Migeyo katika G. Mutahaba, Portrait of a Nationalist: The Life of Ali Migeyo, East African Publishing House, 1969 ndani ya kitabu hicho utapata pia habari za wazalendo wengine kama Sued Kagasheki.
[12] Yusuf Chembera na Salum Mpunga ni waasisi wa TANU Lindi 1956 Mpunga ndiyo aliyomfuata Mwalimu Nyerere Dar es Salaam kuuomba aende Lindi kuhamasisha wananchi kuhusu TANU ni ni wao waliomjulisha Nyerere kwa Sheikh Yusuf Badi.
[13] Hamisi Taratibu na Omar Suleiman ni waasisi wa TANU Dodoma mwaka 1955. Mzee Omar Suleiman amweka kama kumbukumbu kitanda alichukuwa akilalia Mwalimu Nyerere nyumbani kwake wakati wa harakati.
[14] Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 ilitokea sintofahamu baina ya Kasella Bantu na Nyerere na Kasella Bantu akawekwa kizuizini na alipotoka akakimbia nchi kwenda kuishi Ujerumani.
[15] Japhet Kirilo ndiyo alikuwa Mtanganyika wa kwanza kuhutubia Umoja wa Maataifa katika Mgogoro wa Ardhi ya Wameru mwaka 1952. Angalia Kirilo Japhet and Earle Seaton, The Meru Land Case, Nairobi, 1966. Abdulwahid Sykes akiwa katibu wa TAA ndiye aliemsimamia Kirilo kupata hati ya kusafiri kwenda New York baada ya serikali ya kikoloni kumkatalia kumpa pasi. Katika mgogoro huu TAA ilishirikiana kwa karibu sana na Meru Citizen’s Union chama kilichoundwa na watu wa Meru kusukuma mbele madai yao.
[16]Judith Listowel, The Making of Tanganyika, London, 1965.
[17] Kivukoni Ideological College, Historia ya Chama Cha TANU 1954-1977,Dar es Salaam, 1981.

