Home » , » Uhuru wa Tanganyika Haukuletwa na Nyerere Peke Yake Mohamed Said

Uhuru wa Tanganyika Haukuletwa na Nyerere Peke Yake Mohamed Said

Written By mahamoud on Monday, 30 December 2013 | 11:39


Uhuru wa Tanganyika Haukuletwa na Nyerere Peke Yake

Mohamed Said

Kama kawaida ya makala za Mzee wangu Yusuf Halimoja huwa ni mchuzi wenye viungo vingi, hiliki, giligilani, abdalasini, binzari nyembamba na kadhalika. Mzee Halimoja kazungumza kuhusu historia ya TANU na nafasi ya Nyerere, kazungumza kuhusu Mihadhara ya “Uchochezi ya Waislam,” kazungumza kuhusu Elimu ya Waislam na Chuo Kikuu, kama ada yake hakuweza kuacha kuzungumza kuhusu Waarabu na Utumwa, nk. (Jamhuri 17 23, 2012) Insha Allah nitajitahidi kugusa kote. Pili ningependa kumfahamisha Mzee Halimoja kuwa hicho kichwa kilichopamba makala yangu aliyoijibu, “Halimoja ana Chuki na Waislam,” si kichwa nilichoandika mimi. Nadhani kichwa hiki ndicho kilichomfanya Mzee Halimoja aseme kuhusu “uchochezi” wangu. Sasa ikiwa mimi sikuweka kichwa hicho hapo awali ni wazi kuwa shutuma ya uchochezi itakuwa imeniepuka isipokuwa nitabakia na lile la kuwaenzi Waislam na mchango wao katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Hata hivyo hilo halinitoi katika kujibu baadhi ya shutuma kuhusu Waislam kuwa ni “wachokozi.”

Napenda kumfahamisha Mzee wangu Yusuf Halimoja kuwa kuwa katika maandiko yangu yote na katika mihadhara niliyopata kutoa ndani na nje ya nchi sijapata kusema kuwa Waislam walitoa mchango mkubwa kuliko mchango alitoa Nyerere katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Sijaona haja ya kupima nani kasaidia zaidi harakati za kudai uhuru labda kwa kuwa hata kama leo nitataka kufanya hivyo tatizo litakuwa ni vigezo gani nitumie ili kujua nani kamzidi nani. Hii bila shaka itakuwa kazi kubwa kwa kuwa walipogania uhuru wa Tanganyika walikuwa wengi. Kuna wale waliokuwa pale Makao Makuu ya TAA na kasha TANU pale New Street, Dar es Salaam na kuna wale waliokuwa majimboni. Jingine ni kuwa hadi TANU inaanzishwa TAA ilikuwa tayari ishakuwapo kwa miaka 21 na viongozi wakiingia na kutoka na kila mtu alikuwa na mchango wake. Mzee Halimoja akitaka kujua mchango wa viongozi hawa ambae yeye hawaoni kuwa ni wanasiasa na asome tahariri alizokuwa akiandika katika miaka ya 1930 ndani ya gazeti lake alilokuwa kilihariri yeye mwenyewe, “Kwetu.” Nakala za gazeti hili zinapatikana Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Fiah alikuwa mfuasi wa Marx na alijaribu kuhamasisha tabaka la wafanyakazi na wakulima kuwaunganisha dhidi ya ukoloni. Kuanzia mwaka wa 1950 kulikuwa na kamati ya ndani ya TAA iliyokuja kuasisi TANU. Pamoja na haya kuna viongozi wa Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika waliokujatoa uongozi katika TANU. Sasa vipi mtu atasema harakati kazianza Nyerere wakati haya yalipokuwa yakitendeka Nyerere hakuwapo?  Kuna wazalendo kama Kleist Sykes, Ali Jumbe Kiro,  Ali Mwinyi Tambwe, Salum Abdallah, Ibrahim Hamisi, Hassan Machakaomo Maalim Popo Saleh na wengine, hawa waliitumikia African Association, kasha TAA na baadae TANU. Wengi wao walishughulika sana katika miaka ya 1940 hadi kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili. Kuna watu kama Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz  (wanakamati ya ndani ya TAA) waliokuja kupokea kijiti kutoka kwa wazee wao. Dossa alikuwa hapandi jukwaani lakini ndiyo ilikuwa “benki” ya TANU. Inasemekana hakuna wa kumfikia Dossa kwa fedha alizotoa katika kupigania uhuru. Ikutoshe tu kuwa gari la kwanza TANU kuwanalo kumsaidia Nyerere kwenda huku na kule alilitoa Dossa. Abdulwahid Sykes hakuwa anapanda jukwaani lakini na yeye alikuwa “sanduku la fedha” la TANU, halikadhalika mdogo wake Ally Sykes.

Kalamu ya Abdulwahid Sykes na mipango alokuwa akiipanga akishirikiana Mufti wa Tanganyika na Zanzibar Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu, Dk. Vedasto Kyaruzi, Stephen Mhando na wanakamati wa TAA Political Sub Committee ndiyo iliyosababisha uhuru upatikane mwaka 1961. Kamati hii iliundwa 1950 ndani ya TAA na wakati ule Nyerere hakuwapo. Vijana hawa walikungwa mkono na wazee waliounda Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa na Waislam watupu. Katika hawa wazee wapo waliokuwa wanapanda majukwaani na kusafiri na Nyerere vijijini kuitangaza TANU kama Sheikh Suleiman Takadir, Rajab Diwani na wengineo na walikuwapo wengine hawakuwa wapanda majukwaa lakini wakichangia juhudi zile kwa njia nyingine. Katika hawa mchango wa Mshume Kiyate ni wa kupigiwa mfano. Harakati za kudai uhuru hazikuanza na Nyerere mwaka 1954 vuguvugu lilianza toka miaka ya mwisho ya 1920 African Association ilipoasisiwa. Chama hiki kina historia yake na kina mashujaa wake waliofanya makubwa, katika wakati wao kama Kleist Sykes, Erika Fiah, Ali Juma Ponda, Hassan Tawafiq Suleiman, Edward Mwangosi na wengine wengi. Wazalendo hawa walikuwa na mchango wao wa kuwaamsha wananchi wajijue.


Naamini Mzee wangu Halimoja labda hakuwa anayajua haya kama Watanzania wengi walivyokuwa gizani katika historia hii ya kutukuka. Mzee Halimoja yeye anaamini hapakuwa na siasa katika TAA lakini Waingereza wakijua fika kuwa TAA ingawa haikuwa na katiba ya siasa lakini kilikuwa chama cha siasa kamili. Moja ya masikitiko yangu ni kuwa hadi leo watoto wa marehemu Abdulwahid Sykes hawajaamua kuzifungua na kuziweka wazi shajara zake alizokuwa akiziandika wakati kabla na baada ya kuunda TANU kwa hiyo mengi hayajulikani kama ambavyo tungelipendfa kufahamu. Ningependa kumwekea msomaji hapa machache kutoka nyaraka za Sykes:


 "...it is reported that the Secretary of the Association, Abdul Wahid Sykes has 
dispatched letters to all branches asking members for suggestions under
the following heads for a memorandum to be prepared for the Royal
Commission..."

“...Abdul Wahid Kleist Sykes, Secretary of the African Association who, as

reported in last month's summary (paragraph 20) was going on safari up 

country, visited Mwanza, where he met Paul Bomani, President of the
Bukoba African Association, and accompanied him to Bukoba. Sykes then
visited Kampala alone.....on 8th March, a secret   meeting was held, attended
by leading members of the Mwanza Branch...”

(Tanganyika Political Intelligence Summary March, 1952).


Tukija katika TAA hasa kuanzia mwaka wa 1950 kuna wengi waliopambana na ukitaka kujua hali ya siasa ilivyokuwa wakati ule pitia nyaraka za marehemu Abdulwahid Sykes. Utakayosoma katika nyaraka hizi zitakudhihirishia bila hofu wala wasiwasi kuwa TAA kilikuwa chama cha siasa. Kutokana na nyaraka hizi mwandishi ameandika kitabu cha maisha ya Abdulwahid Sykes na ndani yake kawataja wale wote walioondolewa aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya katika historia ya kudai uhuru. Inawezekana watu kama Halimoja hawataki tu kusikia upande mwingine wa historia. Hili ni jambo la kusikitisha kwani kwa kuifunga akili yao kuhusu historia hii watapitwa na mengi. Halimoja anasema Nyerere ndiye aliyepeleka harakati vijijini. Halimoja anasema hivyo kwa kuwa labda kama ni mkweli kuna asiyoyajua kuhusu kuipeleka TANU kwa wananchi. Ushahidi wa kihistoria haukubaliani na msimamo wa Mzee Halimoja. Ningependa kumkumbusha Mzee Halimoja majina ya waasisi wa African Asociation kwa kuwa yeye kanasa na Cecil Motola peke yake mtu wa Masasi mwenzake. Kleist Sykes ndiye aliyeasisi Africa Association baada ya kuifanyia kazi fikra aliyopewa na Dr. Aggrey mwaka 1924. Kleist aliasisi African Association mwaka 1929 akiwa na rafiki zake wa karibu kama Mzee bin Sudi, ambaye wazazi wake walikuwa Wamanyema kutoka Belgian Congo, Ibrahim Hamis - Mnubi ambaye baba yake alitoka Daffur nchini Sudan, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima - Mzaramo, Suleiman Majisu, Raikes Kusi, Rawson Watts na Cecil Matola - Myao kutoka Masasi, Kleist akiwa katibu muasisi wa African Association.    

Napenda tena kumjuvya Mzee Halimoja kuwa wanachama wa kwanza wa TANU walitoka Rufiji mwaka 1954 na aliyekwenda kuwatafuta wanachama hao ni Said Chamwenyewe baada ya kuagizwa na Abdulwahid Sykes ili TANU ipate tasjila kwa kuwa wakoloni walikataa kuisajili TANU ati chama hakina watu. Katika kipindi hicho majuma machache tu tangu TANU iasisiwe Zuberi Mtemvu akachukua kadi za TANU kutoka kwa Ally Sykes akifuatana na Nyerere wakenda Morogoro kukitangaza chama. Mwaka 1956 katika vijiji vya Dodoma TANU iliingizwa vijijini na Haruna Taratibu na Omar Suleiman. Mwaka huo huo katika vijiji vya Jimbo la Kusini, TANU iliingizwa vijijini na Salum Mpunga, Yusuf Chembera, Suleiman Masudi Mnonji, Shariffa bint Mzee, Said Alley Mwalimu, Mohamed Ali Abdallah na wanaharakati wengine. Huko Kilimanjaro TANU ilienezwa na akina Yusuf Olotu, Mama bint Maalim, Halima Selengia, Melkezedek Saimon, Gabrieli Malaika, Eikaeli Mbowe, Juma Ngoma na wengine wengi. Mifano naweza kuitoa mingi sana.

Halimoja anasema labda kwa kegemea historia ya Nyerere kama aijuavyo yeye kuwa tawi la Dar es Salaam la TANU ndilo lilikuwa dhaifu. Sijui anakusudia tawi lipi kwa kuwa matawi ya TANU Dar es Salaam yalikuwa lukuki na yote hayo yalikuwa na nguvu sana kuanzia Makao Makuu New Street hadi uje Tawi la Kisutu ambalo baadae lilikuja kuhamia Mtaa wa Mvita. Hili tawi la Mvita lilikuwa chini ya uongozi wa Mtoro Kibwana kama katibu na Sheikh Haidar Mwinyimvua kama Mwenyekiti na baadae uenyekiti ukashikwa na Yahya Saleh. Inasemekana tawi hili ndilo lililokuwa na nguvu kushinda matawi yote Tanganyika. Huu ndiyo ukweli na picha na nyaraka kuthibitisha haya yote zipo na mwandishi katika kutafiti historia ya uhuru wa Tanganyika kapata bahati ya kuzisoma nyaraka za wakati huo na kuzifanyia uchambuzi. Sasa kama Mzee Halimoja bado kaelemewa na ile propaganda kuwa TAA kilikuwa chama cha starehe hakuna wa kumzuia katika fikra zake hizo. Kwa mukhtasari hii ndiyo ilikuwa michango ya baadhi ya wazalendo ambao hadi leo taifa limewasahau. Katika hali kama hii vipi Mzee Halimoja atadai kuwa Nyerere alikuwa na mchango wa pekee? Hiyo pekee kama ipo na ataufahamishe tupo tayari kumwazima masikio yetu.

Nampa chamgamoto Mzee Halimoja aeleze ni akina nani waliingiza TANU Peramiho na Masasi. Mtu mmoja asingeweza kupigana vita ile peke yake. Nyerere hakuwa peke yake si Dar es Salaam wala huko vijijini alikosema Mzee Halimoja. Tabu ya wanaotaka kumtukuza Nyerere peke yake kama Mzee Halimoja iko hapa. Wao hawawataki kabisa kusikia historia ya waliomtangulia Nyerere katika siasa au aliokuwanao pamoja bega kwa bega. Hamu yao kubwa ni kuwa historia ya uhuru wa Tanganyika ianze na kumalizikia kwa Nyerere. Iwe itakavyokuwa mimi sina ugomvi na wao kila mtu ana uhuru wa mawazo yake hatulazimishani katika hilo. Jambo la kushangaza ni kuwa anapokuja mtu na maelezo mengine ya historia ya kudai uhuru hawa wenzetu wanaumwa sana. Ninachosema siku zote ni kuwa uhuru wa Tanganyika umepiganiwa kwa kiasi kikubwa sana na Waislam na jambo la kusikitisha hao walioupigania uhuru huo bega kwa bega na Nyerere hawatambuliwi na hawajapewa heshima na hadhi wanayostahili. Haya ndiyo mambo mawili ambayo nimekuwa nikikisisitiza siku zote.

Sasa tuje suala la mihadhara. Historia ya mihadhara ni ndefu na inahitaji makala maalum ili kuitendea haki. Wachungaji walikuwa wakipita katika nyumba za Waislam kuwahubiria wakumkubali Yesu ili waokoke. Hili limekuwa likifanyika kwa zaidi ya  miaka mia sasa. Kuna kisa maarufu cha Sheikh Idrissa bin Saad na padre kutoka kanisa la Misheni Kota aliyekuwa akija nyumbani kwa Sheikh Idrissa kumuhubiria “Neno la Bwana.” Inasemekana Sheikh Idrissa alikuwa akimkaribisha huyu mchungaji na akiagiza chai iletwe kwa jili ya mgeni wake na sheikh akikaa kimya kumsikiliza hadi amalize mahubiri yake kisha wanaagana. Wanafunzi wa sheikh walikuwa wakikereka sana na hali ile lakini Sheikh Idrissa alikuwa akiwaeleza kuwa dini inahitaji ustahamilivu. Kwa muda mrefu sana mahubiri ya dini yalikuwa yakifanywa na Wakristo peke yao na kwa kweli mihadhara hiyo haikuwa na athari yoyote kwenye Uislam. Matatizo yalianza pale Waislam kuanzia miaka ya mwanzo 1990 nao walipoanza kutoka misikitini na kuutangaza Uislam hadharani wakitumia Biblia. Baada ya mihadhara hii huko Sumbawanga Wakristo 2000 kutoka Kanisa Katoliki walisilimishwa na Kagera Padri Yusufu Makaka wa Kanisa la Kilutheri Kagera yeye na wafuasi wake 3000 walisilimu na kuingia Uislam. Hofu kuu iliingia katika kanisa na hawakuwa na pa kwenda isipokuwa kuomba msaada wa seriakali ilihami kanisa lisije likasambaratika. Kadinali Otunga wa Kanisa Katoliki Kenya yeye alitoa ilani kwa kusema kuwa kanisa lipo katika hali ya kusambaratishwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kulihami dhidi ya wahubiri wa Kiislam. Kufuatia matokeo haya mwaka 1989 Christian Council of Tanzania (CCT) iliionya serikali kuhusu wahubiri wa Kiislam.  Mwaka 1993 Tanzania Episcopal Conference (TEC) ikatoa taarifa yenye vitisho kuwa endapo Waislam hawataacha mahubiri yao damu itamwagika.  Mapdri walijaribu kupambana na wahubiri wa Kiislam juu ya ulingo lakini walikuwa wanashindwa vibaya sana. Hilo ndilo lilowafanya wakimbilie kutoa vitisho na kutaka msaada wa serikali kuwadhibiti Waislam. Mtokeo ya juhudi hizi za kanisa ni mauaji ya Mwembechai mwaka 1998. Hii ndiyo hali ya mambo kwa mukhtasari.

Mzee Halimoja kaeleza habari ya Waarabu na utumwa. Hakuna wa kupinga hilo kuwa Waarabu walishiriki katika biashara ya utumwa kama vile walivyoshiriki Wazungu na Waafrika. Hata hivyo ningependa kumzindua kuwa mbona kawataja Waarabu peke yao katika biashara hii? Kwani yeye hajui kuwa kulikuwa na biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlantic na meli  moja ya kubeba watumwa ilikuwa ikiitwa “Jesus?” Mzee Halimoja kaeleza Waislam kukosa chuo kikuu hadi walipopewa na Benjamin Mkapa. Kisa cha East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kupigwa kwake marufuku na Nyerere ni katika mambo maarufu kwa Waislam. Mzee Halimoja anatonesha kidonda. Nyerere aliihujumu jumuia hiyo ya Waislam kwa kuwa ilikuwa ikijenga Chuo Kikuu. Mkapa akitumia gazeti la Nationalist, Martin Kiama akitumia Radio Tanzania, Geofrey Sawaya wa Jeshi la Polisi walikuwa washiriki wakuu wa katika kampeni ile dhidi ya EAMWS mwaka 1968 kama lilivyokuwa Kanisa Katoliki wakimtumia Nyerere. Hii ni mada ya kujitegemea Insha Allah itakapopatikana nafasi tutazungumza kwa marefu na mapana yake.


Mwisho ningependa kumwekea Waislam waliopata misukosuko wakati wa utawala wa Nyerere. Nafanya hivi kwa kuwa yeye anadai Waislam hawakutaabishwa na Waingereza. Ukweli ni kuwa Waingereza na Watanganyika waliendesha siasa za upole tofauti na Kenya. Matatizo kwa Waislam na Uislam yalikuja baada ya uhuru mwaka 1961. Hawa wafuatao ndiyo waliofungwa na Nyerere:Abdillah Schneider Plantan, Sheikh Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Shariff Hussein Badawiy, Shariff Mwinyibaba, Shariff Adnan, Bilali Rehani Waikela, Sheikh Jumanne Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh Hashim Haji Abdallah, Sheikh Nurdin Hussein, Salum Abdallah Popo (babu yake Mwandishi), Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al Amin Maftah, Rajab Kiguu cha Mbuzi, Ahmed Rashad Alina wengine wengi.

Juu ya hayo yote Tanzania ni nchi huru watu wana uhuru wa kumpachika yeyote wampendae jina wanaloona linamwenea ama liwe “Baba wa Taifa,” “Baba wa Kanisa” nk. Mtu huwezi kuwa na ugomvi na mambo kama haya. Leo kuna maprofesa wala hawajauona mlango wa darasa na maprofesa hawajaenda mahakamani kuweka p;ingamizi wala wenye shahada zao hawajaonesha kukereka.  Ukipenda unaweza hatakuwa Field Marshal na hakuna atakaekuuliza wapi ulipigana vita na katika jeshi lipi.  Halikadhalika mtu ana uhuru wa kuamini historia yoyote aitakayo. Anaweza kudai kuwa TANU ilianzishwa na Nyerere mwaka 1954 na akaja mwingine akasema hilo haliwezekani na kama kuna mzalendo anaeweza kujinasibu na kuanzishwa kwa TANU basi marehemu Abdulwahid Sykes anastahili zaidi kwani baba yake ndiye aliyeasisi African Association mwaka 1929 na kati ya 1930 hadi 1933 akajenga ofisi ya African Association New Street, nyumba ambayo TANU ilikuja kuzaliwa ndani yake mwaka 1954.

Siwezi kumjibu Mzee Halimoja kila alosema hapa tulipofika panatosha.
19 Januari, 2012

Sheikh Nurdin Hussein Khallifa wa Tariqa Shadhliy 
Ali Juma Ponda
Erika Fiah

Share this article :

Post a Comment

Unadhani kuwa nani anasifa ya kuwa rais wa Tanzania?