Home » , » DK. VEDASTO KYARUZI DAKTARI MWANAHARAKATI WA TAA

DK. VEDASTO KYARUZI DAKTARI MWANAHARAKATI WA TAA

Written By mahamoud on Thursday, 26 December 2013 | 04:19

DK. VEDASTO KYARUZI DAKTARI MWANAHARAKATI WA TAA

Na Mohamed Said

Utangulizi

Katika moja ya misiba mikubwa iliyoikumba Tanzania ni kukosekana kwa historia inayoweza kuaminika kuhusu mashujaa wake waliopigania uhuru kutoka kwa Waingereza. Gazeti la Raia Mwema (Mei 23 - Mei 29, 2012) limefahamisha umma kuhusu kifo cha Dk. Vedasto Kyaruzi na kwa muhtasari wakaweka sifa zake. Kwa bahati mbaya sana sifa walizoweka hazikuwa za kweli kwa kiasi fulani. Mfano ni pale makala iliposema Dk. Kyaruzi ndiye aliyemwachia uongozi Nyerere katika TAA na kuwa alikuwa rais wa kwanza wa TAA. Ukweli ni kuwa Nyerere na Dk. Kyaruzi hawakupata kukutana katika uongozi wa TAA kwa hiyo isingewezekana kwa Dk. Kyaruzi kumwachia Nyerere uongozi. Wakati Nyerere anaingia TAA Makao Makuu, Dar es Salaam mwaka 1952 Kyaruzi alikuwa keshaondoshwa  Dar es Salaam na wakoloni kapelekwa Nzega na chama kilikuwa chini ya uongozi wa Abdulwahid Sykes akiwa katibu na kaimu rais. Abdulwahid ndiye aliyeikabidhi TAA kwa Nyerere mwaka 1953. Jingine ni kuwa Kyaruzi wala hakuwa rais wa kwanza wa TAA kwani chama kilianzishwa Dar es Salaam mwaka 1929 kikijulikina kama African Association na wakati huo Dk Kyaruzi alikuwa bado mtoto mdogo. Mwaka wa 1948 ndipo kilipokuja badilishwa jina na kuitwa Tanganyika African Association (TAA) Kwa nia njema kabisa naweka hapa maisha ya siasa ya Dk. Kyaruzi kama nilivyoyaandika katika moja ya sura za kitabu changu “Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes 1924 - 1968...” Katika makala haya nimefanya mabadiliko hapa na pale ili kumwezesha msomaji kufuatilia siasa za TAA kama zilivyokuwa wakati wa uongozi wa Dk. Kyaruzi mwaka wa 1950.


 Juhudi za Kubadili Uongozi Mkongwe wa TAA Uliochoka, 1949 - 1950

Kwa miongo miwili kuanzia mwaka wa 1929 Chama cha African Association kilikuwa mikononi mwa viongozi watu wazima sana mfano wa Mzee bin Sudi na Mwalimu Thomas Sauti Plantan ambae alikuwa rais wa chama hicho mwaka wa 1949. Mzee bin Sudi na Kleist Sykes walipata vilevile kuwa rais na katibu wa African Association na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika kwa wakati mmoja katika miaka ya 1930. Vyama hivi viwili vilikuwa vikifanya harakati zake kwa karibu na ushirikiano mkubwa kwa kuwa viongozi wake walikuwa viongozi wa ngazi ya juu katika vyama hivyo viwili. Siasa za kikoloni zilikuwa zikibadilika na kwa hivyo zilihitaji damu change kama za akina Dk. Kyaruzi zenye mawazo na mbinu mpya ili kuongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Serikali ya kikoloni ilikuwa kila uchao inabadili mitindo, hila na mbinu za ukandamizaji ili kuendeleza utawala wake. Ukitazama mwelekeo wa siasa na mazingira ya wakati ule, uongozi wa wazee katika African Association, kwa hali yao na kutokana na mambo yalivyokuwa yakiwakabili, walikuwa hawana uwezo wa kukabiliana na changamoto ya ukoloni. Lakini pamoja na yote hayo, wazee hawakutaka kuachia madaraka. Jambo hili lilizusha mvutano baina ya wazee na wanasiasa vijana. Vijana hawa walikuwa akina Abdulwahid na Ally Sykes (ambao baba yao, Kleist Sykes ndiye aliyeasisi African Association), Tewa Said Tewa, Stephen Mhando, Waziri Dossa Aziz, James Mkande, na wale madaktari watano - Vedasto Kyaruzi, Joseph Mutahangarwa, Luciano Tsere, Michael Lugazia na wengineo. Haya yalikuwa ni mapambano baina ya kizazi kipya na kile cha kale. Vita Kuu ya Pili ilikuwa imemalizika na ukoloni katika Tanganyika sasa ukawa unakabiliwa na changamoto mpya kutoka kwa vijana wasomi toka Chuo cha Makerere na askari wa Tanganyika waliopigana Burma katika Vita ya Pili Vya Dunia chini ya King’s African Rifles (KAR).

Katika mvutano huu wa madaraka kwa upande wa vijana waliokuwa wakiinukia alikuwepo kijana wa Kidigo kutoka Tanga aliyehitimu Makerere, Hamza Kibwana Mwapachu. Mwapachu alikuwa ameajiriwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii kama 'Assistant Welfare' Officer (Msaidizi wa Ustawi wa Jamii), Ilala Welfare Centre mjini Dar es Salaam. Historia ya Mwapachu katika siasa ilianza Makerere College, Uganda ambako alijihusisha na mambo ya siasa wakati alipokuwa mwanafunzi. Mwaka wa 1947 Mwapachu akiwa Tabora alichaguliwa kuwa katibu wa African Association, Julius Nyerere akiwa naibu wake. Mwapachu na Abdulwahid walikuwa na usuhuba mkubwa. Mwaka wa 1950 Mwapachu alikuwa na umri wa miaka 32 na Abdulwahid alikuwa na umri wa miaka 26, mdogo kwa Mwapachu kwa miaka sita. Vijana hawa wawili walikuja kugeuza mwelekeo wa TAA na wakaingiza ndani ya chama hicho aina mpya ya uongozi na ushawishi uliokuwa haujapata kuonekana katika historia ya Tanganyika. Lakini wote wawili walifariki dunia katika ujana wakiwa na umri wa miaka 44 tu. Na wote wawili wakaja kusahauliwa na historia. Hakuna kati yao ambaye hii leo jina lake linahusishwa na historia ya Tanganyika ingawa wao ndiyo waliomvuta Nyerere katika TAAna  siasa za Dar es Salaam ya miaka ya mwanzo ya 1950. Kupitia vijana hawa wawili ndipo historia ya Dk. Kyaruzi ilipoanza. Uongozi wake ulikuwa mfupi katika TAA lakini uongozi huo ulifanya makubwa na kubadilisha sura ya harakati. Katika siku zake za mwisho Dk. Alipata kumwambia mmoja wa watoto wa Hamza Mwapachu kuwa, “Kama si mipango waliyoweka baba yako na Abdulwahid mwaka 1950 tusingelipata uhuru mwaka 1961.”

Ofisi ya Mwapachu pale Ilala ilikuwa kituo cha mijadala ya siasa nyakati za mchana.  Jioni vikao hivyo vya majadiliano vilihamia Tanga Young Comrades Club. Hiki ilikuwa kilabu maarufu ya vijana wa mji kukutana. Kilabu hii ilikuwa New Street (sasa Mtaa wa Lumumba) karibu na ofisi ya TAA. Mijadala ya siasa nyumbani kwa Abdulwahid au katika ofisi ya Mwapachu Ilala au Tanga Club kidogo kidogo ikawa inaingia katika nadharia ya vipi vijana wangeweza kuuondoa madarakani uongozi wa Mwalimu Thomas Sauti Plantan ndiye aliyekuwa rais wa katibu wake Clemet Mohammed Mtamila.

Si kwamba Tanganyika wakati ule ilikuwa na uhaba wa maswala ambayo yangeweza kuamsha mijadala ya siasa. Kulikuwa na mambo kadhaa ambayo kama yangetumiwa kwa ustadi na uongozi wa TAA, shida hizo zingeweza kuleta kwa watu hisia za manung’uniko na chuki dhidi ya serikali ya kikoloni. Vitu ambavyo TAA ingeweza kuvitumia kuwafitini Waingereza dhidi ya wananchi. Unahitaji tu kuzipitia tahariri za Ramadhani Mashado Plantan katika gazeti lake alilokuwa akihariri mwenyewe lililojulikana kama “Zuhra” ili kuweza kufahamu siasa ilivyokuwa ikitokota chini kwa chini Tanganyika katika miaka ya 1950. Rais wa TAA Mwalimu Thomas Plantan na damu yake ya Kizulu ya kupenda vita, baada ya kuwa yupo kwenye nchi yenye amani, aliielekeza bunduki yake porini kuwinda wanyama. Hakuwa na muda kama rais wa TAA kushughulika na masuala ya TAA. Uhodari wake katika kuwinda bado hadi miaka ya 1970 iliweza kushuhudiwa nyumbani kwake Mtaa wa Masasi, Mission Quarters. Kuta za nyumbani kwake zilikuwa zimepambwa na mafuvu ya vichwa vya wanyama aliowaua huko porini Mwalimu Thomas Plantan hakuwa na muda wa kuitisha mikutano au kushughulikia mambo ya TAA kwa sababu alitumia wakati wake mwingi porini. Makao Makuu ya TAA mjini Dar es Salaam yalikuwa kama vile yamegubikwa na usingizi mzito. Barua kutoka matawini hazikuwa zikijibiwa. Baya zaidi, hakukuwepo na mawasiliano yoyote na Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, mjini New York ambalo ndilo lilikuwa likiitawala Tanganyika kama nchi ya udhamini. Juu ya haya ndani ya TAA na uongozi wake kulikuwa na hali na sura nyingi za ukinzani. Schneider Abdillah Plantan mmoja wa viongozi wa TAA alikuwa siku nyingi amekwishaonyesha chuki yake dhidi ya Waingereza na kwa ajili hiyo akawekwa kizuizini wakati wa Vita Vya Pili kwa kuonyesha msimamo wa kumuunga mkono Hitler dhidi ya Waingereza. Yeye mwenyewe mwaka 1914 alipigana Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya Waingereza akiwa askari katika jeshi la Wajerumani akiwa na ndugu yake Kleist Sykes (wakati ule akijulikana kama Kleist Plantan), Mashado Plantan alikuwa na gazeti lake “Zuhra” ambalo lilikuwa ndiyo sauti ya African Association. Lakini watu hawa walikuwa wazee na wamechoka. Hawakuwa na jipya katika siasa mbali na kuuchukia utawala wa kikoloni.

Walipochoshwa na uongozi huu wa wazee na walipoona hakuna lolote la maana liliokuwa siku moja wakati wa alasiri, Abdulwahid na Mwapachu bila ya kumshauri mtu yeyote wakitokea Tanga Club, New Street, walivamia ofisi ya TAA na kufanya mapinduzi kwa kumtoa msobe msobe Clement Mtamila ofisini kwake. Abdulwahid alikuwa bingwa wa ngumi wa Tanganyika na Kenya katika kikosi chake wakati wa vita. Hakupata tabu sana kumtoa nje ya ofisi Mtamila. Baada ya vurugu hii ambayo ilikuwa gumzo la mji kwa wakati ule wazee walisalimu amri na wakaamua kuitisha uchaguzi. Maofisa Wazungu kutoka serikalini walihudhuria mkutano huu kama mbinu ya kuwatisha vijana waliokuwa wakishinikiza mageuzi katika TAA. Bila woga Schneider Plantan aliwakabili na kuwaeleza kuwa uchaguzi utafanyika watake wasitake. Shneider alipigwa risasi mguuni vitani kwa hiyo alikuwa akichechemea. (Katika moja ya sifa zake ni kuwa alikuwa mtu shujaa sana. Hamuogopi yeyote. Shneider ndiyo mtu pekee katika historia aliyesimama uso kwa uso na Nyerere na Shneider akamtukana Nyerere nyumbani kwake Msasani huku akimtazama usoni). Mwezi Machi mwaka 1950, katika Ukumbi wa Arnatouglo, kijana wa Kihaya, Dk. Vedasto Kyaruzi alichaguliwa kuwa rais wa TAA na Abdulwahid Sykes katibu wake. Dk. Kyaruzi alipochukua uongozi, TAA ilikuwa na shilingi 87.00 Barclays Bank, Dar es Salaam. Huu ndiyo ulikuwa mwisho wa wazee, kuongoza TAA. Vilevile ndiyo ukawa mwanzo wa uzalendo na utaifa Tanganyika. Abdillah Schneider Plantan na mdogo wake Ramadhani Mashado Plantan walimuuunga mkono Dk. Kyaruzi katika kuipa TAA uhai mpya ingawa aliyetolewa madarakani alikuwa kaka yao mkubwa Mwalimu Thomas Sauti Plantan. Hivi ndivyo Dk. Kyaruzi alivyoingia katika uongozi wa TAA.

Dk. Kyaruzi Katika Kamati Ndogo ya Siasa Ndani ya TAA, 1950 -1951

Hakuna nyaraka zozote zinazoonyesha kama African Association ilikuwa imetayarisha mpango wa kushughulikia hali ya siasa.  Kuelewa mwelekeo wa siasa wakati ule inabidi mtu atazame mwenendo wa viongozi wa TAA na jinsi walivyokuwa wakiyashughulikia mambo tofauti yaliyokuwa yakiwadhili wananchi. Jambo la kwanza walilofanya Dk. Kyaruzi na Abdulwahid Sykes mara tu baada ya kuingia madarakani ni kuunda TAA Political Subcommittee (Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA) iliyomjumuisha Sheikh Hassan bin Amir kama mufti wa Tanganyika na Zanzibar; Dk. Kyaruzi, Mwapachu, Said Chaurembo aliyekuwa liwali wa mahakama ya Kariakoo; John Rupia na Stephen Mhando. Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kushughulika na masuala yote ya siasa katika Tanganyika. Kuundwa kwake ndiyo hasa ulikuwa mwanzo wa siasa za dhahiri katika Tanganyika na mwanzo wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Kwa kipindi cha miaka ishirini na moja African Association ilifanya kazi chini ya katiba isiyokuwa ya siasa. Kwa mara ya kwanza mwaka 1950, TAA chini ya uongozi mpya, ilijipa hadhi ya chama cha siasa, siyo kwa kubadilisha katiba yake bali kwa kuunda kamati ya siasa ndani ya chama. Kamati hii ilikuwa na watu wenye kuwakilisha maslahi na uwezo tofauti, wakiwa halikadhalika wanatokana na uzoefu na hali tofauti. Sheikh Hassan bin Amir Muunguja alikuwa ndiye mufti wa Tanganyika na aliwakilisha Waislam ambao hasa ndiyo waliokuwa wakiongoza mapambano dhidi ya serikali. Said Chaurembo aliwakilisha Wazaramo wa Dar es Salaam na vitongoji vyake.  John Rupia kutoka Mission Quarter alikuwa mfanya biashara tajiri na mfadhili wa chama. Stephen Mhando Mbondei kutoka Muheza alijulikana kwa misimamo mikali aliwawakilisha wasomi wa Makerere, Dk. Kyaruzi akiwa mmojawapo. Uongozi huu ndiyo ulioweka msingi wa kuundwa kwa TANU chama kilichokuja kung’oa ukoloni wa Waingereza katika Tanganyika. 

Baada ya kuunda kamati hii uongozi wa TAA ulianza kuyaandikia matawi ya TAA ili kuyahuisha. Jambo kubwa lililokabili TAA na ile kamati ya siasa ilikuwa ni hadhi ya Tanganyika kama nchi ya udhamini chini ya Umoja wa Mataifa. Uongozi wa TAA ulimuingiza katika kamati ya siasa Earle Seaton, mwanasheria kutoka Bermuda aliyekuwa akikaa Moshi ili aishauri kamati kuhusu mambo ya sheria ya katiba.  Seaton alitakiwa kuishauri jinsi ya kuliendea shauri la kutaka Uingereza itoe uhuru ili Tanganyika ijitawale yenyewe kwa kuwa nchi hiyo haikuwa koloni, bali nchi chini ya udhanini wa Umoja wa Mataifa. Mwaka wa 1948 Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa tayari lilikuwa limetuma ujumbe wake wa kwanza kuzuru Tanganyika. Lakini hakuna jambo lolote la manufaa lilipatikana kutoka kwa ujumbe huo. Makao Makuu ya TAA mjini Dar es Salaam chini ya Dk. Kyaruzi na Abdulwahid ikiungwa mkono na kamati ya siasa sasa ilikuwa ikiamka kutoka kwenye usingizi mzito. Kilichotakiwa ilikuwa ni kupata maswala yakutoa changamoto kwa akili za wale wasomi vijana. Uongozi wa chama cha TAA haukuwa na haja ya kuangaza mbali. Changamoto ilikuja kwa sura ya Constitutional Development Committee (Kamati ya Mapendekezo ya Katiba) iliyoundwa na Gavana Edward Twining na mgogoro wa ardhi ya Wameru.

Uingereza ilikuwa ikitawala Tanganyika chini ya kifungu 76 na 77 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Kama mamlaka tawala Uingereza ilitarajiwa kuanzisha na kuendeleza maendeleo ya siasa, uchumi na ya kijamii ya Tanganyika hadi kufikia wakati ambao watu wake wangekuwa tayari kujitawala.  Lakini Waingereza walifanya khiyana na hawakutimiza ahadi hiyo. Walijihusisha na kulinda maslahi yao wenyewe ya kikoloni na yale ya watu weupe wachache na wakaendelea kuwapuuza Waafrika waliokuwa wengi na wenye nchi. Labda kwa kuanua ngoma juani, Gavana Twining alikaribisha mapendekezo kutoka kwa watu mashuhuri, vyama vya ustawi wa jamii na Native Authorities, kutaka mapendekezo ya jinsi Tanganyika itakavyotawaliwa. Kamati ya siasa ya TAA ilipeleka mapendekezo yake ambayo yalitiwa sahihi na wajumbe wote wa kamati ya siasa.  Sheikh Hassan bin Amir, Abdulwahid Sykes, Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, John Rupia, Stephen Mhando na Said Chaurembo. Katika taarifa yake ya TAA ya mwaka ya 1950 Abdulwahid aliandika:

“Kwa ajili ya maslahi ya Waafrika na kulinda maslahi ya chama hiki na yale ya jumuiya ya Waafrika kwa ujumla, chama kimeweka wakili atakayeshauri juu ya mambo ya sheria. Wakili huyo ni Bwana E. E. Seaton wa Moshi. Mara kwa mara amekiandikia chama hiki juu ya masuala mbali mbali ya siasa, na kwa kiasi kikubwa ushauri wake umesaidia wakati chama hiki kilipokuwa kikitayarisha mapendekezo juu ya katiba.”

Uongozi wa Dk. Kyaruzi na Abdulwahid ulitambua kuwa matatizo mengi kuhusu haki za Waafrika yalikuwa masuala ya kisheria ambayo yalihitaji ushauri wa wanasheria. Kwa mara ya kwanza kwa msaada wa Seaton, TAA kilitoa hoja zake zilozotiwa nguvu na ukweli  hoja na kwa tarakimu zilizoonyesha udhalimu ndani ya mfumo wa kikoloni ambao ulikuwa kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Memorandum ya TAA kwa Constitutional Development Committee ambayo Pratt amesema iliandikwa kwa utaalamu wa hali ya juu na uongozi wa makao makuu ya Tanganyika African Association ilipendekeza kuwa ndani ya baraza la kutunga sheria  Waafrika watashika  nusu ya viti kwa miaka kumi na mbili na baada ya hapo ipigwe kura kuwachagua wajumbe.

Kufuatia mwamko huu wa chama, serikali ilishtuka na ikaanza kuingia hofu, ikaamua kumpa uhamisho Dk. Kyaruzi, rais wa TAA, kutoka Dar es Salaam kwenda Hospitali ya Gereza la Kingolwira karibu na Morogoro. Serikali ya kikoloni iliamini kwa kufanya hivyo itaweza kupunguza kasi ya TAA katika uwanja wa siasa. Serikali ilidhani kwa kumtoa Dk. Kyaruzi Dar es Salaam, jambo hilo lingedhoofisha uongozi wa TAA pale makao makuu. Lakini Dk. Kyaruzi hakukwazwa na huo uhamisho. Kila mwisho wa juma alisafiri Dar es Salaam kushauriana na Abdulwahid. Serikali ilipotambua kuwa uhamisho huo haukuathiri chochote katika mchango wa Dk. Kyaruzi kwenye uongozi wa TAA, alihamishwa tena kutoka Kingolwira hadi Nzega mbali kabisa na Dar es Salaam. Hapo ikawa Dk. Kyaruzi amepatikana. Dk. Kyaruzi alikuwa sasa yuko kwenye “kifungo kisicho rasmi cha kisiasa” alichogubikwa na Waingereza asijihusishe tena na siasa za kudai uhuru. Dk. Kyaruzi hakurejea tena katika siasa za uzalendo pale Makao Makuu New Street. Waingereza wakafuatia mwaka 1951 na 1953 kwa kutoa sekula za kukataza watumishi wa serikali kujihusisha na siasa wakiwakusudia watu kama Dk. Kyaruzi.

Gavana Twining iliyapuuza mapendekezo ya kamati ya TAA. Serikali iliendelea na mipango yake ya muda mrefu ya kuwaimarisha Wazungu na Waasia waliokuwa wachache na kuwasukuma kando Waafrika kinyume kabisa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zilizokuwa chini ya udhamini. Waafrika wengi wenye elimu walionelea kuwa mapendekezo ya TAA ndiyo yangekuwa msingi wa katiba ya baadaye ya Tanganyika kama jamii ya watu wa rangi zote. Lakini moyo wa mapendekezo yale ya TAA haukufa. Mapendekezo yale yaliletwa tena katika mkutano wa kuanzishwa kwa TANU tarehe 7 Julai, 1954. Mapendekezo hayo ndiyo baadaye yalitiwa katika hotuba ya Julius Nyerere aliyoisoma mbele ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, New York, mwezi wa Machi, 1955. Nyaraka hii imepotea. Haipo katika Maktaba ya CCM, Dodoma wala katika jalada lake na katika “microfilm” ilipohifadhiwa Tanzania National Archive (Nyaraka za Taifa).

Hitimisho

Katika miaka hii ya karibuni nimesoma makala kadhaa ambazo Dk. Kyaruzi akifanyiwa mahojiano na waandishi wa magazeti tofauti na katika kila makala Dk. Kyaruzi hakuacha kuweka msisitizo kuwa yeye ndiye aliyemuachia TAA Nyerere. Hiki ni kitu ambacho mimi kama mtafiti na mwandishi wa historia ya uhuru wa Tanganyika kilikuwa kikinitaabisha sana. Kilichokuwa kikinipa shida ni kuwa nilikuwa nikifahamu kuwa Dk. Kyaruzi aliingia katika uongozi wa TAA mwaka 1950 pamoja na Abdulwahid Sykes. Nilikuwa najua kuwa waliomsaidia kuingia katika uongozi walikuwa watu wa mjini akina Plantan na Sykes. Vipi watu hawa hakuwa anawakumbuka? Wakati Nyerere anachukua uongozi wa TAA mwaka 1953 Kyaruzi hakuwa Dar es Salaam. Hiki ni kitu kikinishughulisha sana. Jambo hili likishighulisha sana fikra zangu kwa kujiuliza mbona Kyaruzi anamruka Abdulwahid Sykes katika historia yao ya uongozi wa TAA mwaka wa 1950 na kumwingiza Nyerere ilhali Nyerere wakati ule hakuwa anafahamika na yeyote katika duru za siasa za Tanganyika? Nikawa nashangaa nikijiuliza kwani Dk. Kyaruzi hajui kuwa Nyerere aliingia katika uongozi wa TAA mwaka 1953? Nilikuwa nikijifariji kwa kusema kuwa haya ndiyo matatizo ya historia ya uhuru wa Tanganyika. Lakini jambo linalonisikitisha sana ni kujua kuwa katika miaka ya 1970 Dk. Kyaruzi alipeleka mswada wa maisha yake kwa mchapaji mmoja wa vitabu ili mswada wake uhaririwe na kuchapwa kitabu. Mchapaji yule ambae lilikuwa shirika la umma lilikataa kuchapa kitabu kile. Sijui kwa nini walikataa kuchapa kitabu kile ambacho kwa hali yeyote ile ingelikuwa hazina kubwa kwa vizazi vijavyo nah ii leo wakati wa umauti wake tungelimjua bila wasiwasi Dk. Kyaruzi na mchango wake katika uhuru wa Tanganyika na jinsi kama alivyosema mwenyewe vipi alimwachia TAA Nyerere.


25 May 2012
Share this article :

Post a Comment

Unadhani kuwa nani anasifa ya kuwa rais wa Tanzania?